Staffan de Mistura: Watu laki nne wameuawa katika vita nchini Syria
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amesema watu wapatao laki nne wamepoteza maisha kutokana na vita vya zaidi ya miaka mitano vilivyoikumba nchi hiyo ya Kiarabu.
Staffan de Mistura, ameyasema hayo mjini Geneva, Uswisi pembeni ya mazungumzo ya amani ya Syria na kubainisha kuwa takwimu hizo ni kulingana na 'upembuzi na uchanganuzi' wake na si takwimu 'zilizothibitishwa'.
De Mistura ametoa takwimu hizo za kuuawa watu wapatao laki nne katika vita na machafuko nchini Syria katika hali ambayo, kutokana na kushindwa kupata taarifa za uhakika, Umoja wa Mataifa umesitisha mchakato wa kukusanya takwimu za idadi ya watu waliouawa katika mgogoro wa nchi hiyo.
Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria ameongeza kuwa watu laki mbili na nusu wameuawa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Takwimu zilizotolewa na De Mistura zinakaribiana na zile zilizotolewa mwezi Februari na kituo cha utafiti wa kisiasa cha Syria. Kwa mujibu wa kituo hicho watu zaidi ya laki nne na elfu sabini wameuawa moja kwa moja na kwa njia ya isiyo ya moja kwa moja katika vita na machafuko ya miaka mitano yanayoendelea nchini Syria.
Ripoti ya kituo hicho cha utafiti wa kisiasa cha Syria aidha imebainisha kuwa watu wapatao milioni moja na laki tisa wamejeruhiwa katika vita na machafuko hayo.
Usitishaji vita unaosuasua wa hivi sasa nchini Syria ulianza kutekelezwa Februari 27 kwa upatanishi wa Russia na Marekani na bila ya kuyajumuisha makundi ya kigaidi na kitakfiri ya Daesh na Jabhatu-Nusra ambalo ni tawi la kundi la kigaidi la Al-Qaeda nchini Syria.../