Nasrullah: Hizbullah inatekeleza jukumu lake, Marekani inazuia utatuzi Lebanon
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon jana Ijumaa alitoa hotuba muhimu katika kumbukumbu za kumuenzi Allama Sayyid Murdha al Amili, mmoja wa maulamaa na wanavyuoni wakubwa wa nchini Lebanon, na mbali na kugusia shakhsia ya mwanachuoni huyo, amezungumzia pia matukio ya ndani ya Lebanon na kujiuzulu waziri mkuu wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Sayyid Hassan Nasrullah amegusia matukio ya ndani ya Lebanon yaliyoanza wiki mbili zilizopita na njama za maadui wa taifa hilo wanaojaribu kuzusha vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na kusisitiza kuwa, Hizbullah ina taarifa kamili kuhusu watu wanaotoa fedha, wanaopokea fedha na wanaojaribu kuitumbukiza Lebanon katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katibu Mkuu huyo wa Hizbullah ya Lebanon amewataka wananchi wa nchi hiyo kuwa macho na kuwa na muono wa mbali akifafanua kuwa, baadhi ya wanasiasa ndani ya Lebanon wanachochea machafuko.
Vile vile ametahadharisha kuhusu kutumiwa vibaya na wanasiasa matakwa ya haki ya wananchi na kutoa mwito kwa viongozi wa kisiasa nchini humo kutowatumia wananchi kama chambo cha kujinufaisha binafsi.
Kuhusu kujiuzulu Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad Hariri, Sayyid Hassan Nasrullah amesema, tangu awali Hizbullah ilitangaza kuwa inapinga jambo hilo na ilipendekeza kwamba serikali ikae na wananchi wanaoandamana na kutatua kwa pamoja matatizo yaliyopo na sio kukimbilia kujiuzulu waziri mkuu na kuvunja baraza la mawaziri.
Vile vile amesema, Marekani ndiyo inayochochea machafuko huko Lebanon na inafanya njama za kusambaratisha uchumi wa nchi hiyo akisisitiza kuwa, hizo si tuhuma, bali ni uhakika wa mambo wenye ushahidi kamili.