HRW: Ukandamizaji Saudia umefika hatua mpya chini ya Bin Salman
Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limesema dhulma, mateso na ukandamizaji umeongezeka na kufikia kiwango kipya cha kutisha nchini Saudi Arabia, tangu Mohammad Bin Salman atangazwe kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.
Ripoti mpya iliyotolewa jana Jumatatu na shirika hilo lenye makao makuu yake mjini New York inasema kuwa, watawala wa Riyadh wameshadidisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani, wanazuoni na wakosoaji wake katika kipindi cha miaka miwili cha utawala wa Bin Salman.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa, ukandamizaji dhidi ya wapinzani na wanaharakati wa haki za binaadamu na wa haki za wanawake sio jambo jipya nchini Saudia, lakini kiwango cha dhulma hizo kiliongezeka mno tangu mwishoni mwaka 2017 baada ya Bin Salman kutangazwa kuwa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo na babake Mfalme Salman.
Mwezi Septemba 2017, miezi michache baada ya Bin Salman kuteuliwa kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, makumi ya wafanyabiashara, wanazuoni wa kidini, wanawafalme, wanaharakati wa haki za binaadamu na haki za wanawake pamoja na maulama wa nchi hiyo walitiwa mbaroni na kutupwa jela; na wimbi hilo la kamatakamata linaendelea kwa kiwango cha kutisha hadi hivi sasa.
Ripoti hii ya Human Rights Watch imetolewa siku chache baada ya watu sita kutiwa mbaroni na maafisa usalama wa nchi hiyo, kwa tuhuma ya kumkosoa mmoja wa watu wa karibu na Mohammad Bin Salman.