Wairaqi walaani vikali kuuawa Qassem Soleimani na Abu Mahdi
Shakhasia mbali mbali wa kisiasa na kidini nchini Iraq wamelaani vikali hujuma ya kigaidi ya Mareknai ambayo imepelekea Meja Jenerali Qassem Suleimani na Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq (Al Hashd al Shaabi) Abu Mahdi la Muhandis kuuawa shahidi.
Hadi al Ameri mmoja kati ya makamanda wa ngazi za juu wa Al Hashd al Shaabi ametoa taarifa na kutoa wito kwa makundi yote ya kisiasa ya Iraq yaungane katika kushinikiza kuondolewa wanajeshi wote wa kigeni Iraq. Amesema uwepo wa wanajeshi wa Marekani Iraq haujaleta chochote isipokuwa umwagaji damu.
Al Ameri amelaani vikali jinai hiyo chafu ya Marekani na kuongeza kuwa, mauaji hayo yatazidisha irada na azama ya kuendeleza jihadi na kujitolea muhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Naye Sheikh Abdul Mahdi Karbalai, mwakilishi wa Ayatullah Sistani, Marjaa wa Kidini Iraq, katika hotuba yake ya Sala ya Ijumaa mjini Karbala amesema kile ambacho kimejiri karibu na Uwanja wa Ndege wa Baghdad ni hujuma ya kinyama ambayo imekiuka mamlaka ya kujitawala Iraq.
Ofisi ya rais wa Iraq pia imetoa taarifa na kuonya kuhusu matokeo mabaya ya kuuawa shahidi Haj Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Haj Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa Hashd al Shaabi. Aidha ofisi ya rais wa Iraq imelaani vikali hujuma hiyo ambayo ilijiri jana Ijumaa.