Kushtadi mashambulizi ya mizinga ya jeshi la Uturuki kaskazini mwa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60330-kushtadi_mashambulizi_ya_mizinga_ya_jeshi_la_uturuki_kaskazini_mwa_syria
Uvamizi wa jeshi la Uturuki katika maeneo ya kaskazini mwa Syria, bado unaendelea na katika uwanja huo vyombo vya habari vya Uturuki vimethibitisha kuendelea mashambulizi ya mizinga ya askari wa nchi hiyo ndani ya maeneo ya taifa hilo la Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 12, 2020 22:23 UTC
  • Kushtadi mashambulizi ya mizinga ya jeshi la Uturuki kaskazini mwa Syria

Uvamizi wa jeshi la Uturuki katika maeneo ya kaskazini mwa Syria, bado unaendelea na katika uwanja huo vyombo vya habari vya Uturuki vimethibitisha kuendelea mashambulizi ya mizinga ya askari wa nchi hiyo ndani ya maeneo ya taifa hilo la Kiarabu.

Kabla ya hapo siku ya Jumatano ya tarehe 8 Aprili mizinga ya jeshi la Uturuki pia ilivilenga viunga vya mkoa wa Aleppo nchini Syria. Licha ya viongozi wa serikali ya Ankara kueleza kuwa mashambulizi hayo yalikusudia maeneo ya kijeshi yaliyoainishwa na kuharibu maeneo hayo, vyombo vya habari vya kujitegemea vimefichua nyaraka za kujiri mauaji dhidi ya wanawake, watoto na wazee wa Syria kutokana na mashambulizi ya jeshi hilo vamizi katika maeneo ya makazi yasiyo ya kijeshi. Ukweli ni kwamba, habari zilizosambazwa na vyombo vya habari vya Uturuki na vile vya kujitegemea zinatofautiana sana. Kwa mfano tu, katika kujiri mashambulizi ya mizinga ya hivi karibuni ya jeshi la Uturuki katika maeneo ya kaskazini mwa Syria, raia kadhaa wa nchi hiyo ya Kiarabu waliuawa. Katika uwanja huo, kituo kinachoitwa 'Haki za Binaadamu nchini Syria' kimeripoti kwamba: "Askari wa jeshi la Uturuki walivishambulia kwa mizinga vijiji vya kaskazini magharibi mwa mkoa wa Aleppo, na kusababisha hasara za kibinaadamu na kifedha kwa jeshi la Syria."

Licha ya njama za Uturuki, Marekani na Israel dhidi ya Syria lakini serikali ya Damascus imeendelea kusimama imara

Kwa hakika, duru hii ya mashambulizi ya jeshi la Uturuki ndani ya ardhi ya Syria, ambayo ni operesheni ya nne ya kijeshi katika nchi jirani, imekabiliwa na malalamiko makali ya ndani, kieneo na kimataifa. Awali jeshi hilo vamizi liliyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Syria kwa kisingizio cha kupambana na magaidi sambamba na kutuma maelfu ya askari wake ndani ya nchi hiyo jirani. Mwanzoni mwa mashambulizi ya jeshi la Uturuki nchini humo, kulisikika katika vyombo vya habari vya kieneo na dunia tuhuma kama vile za mauaji ya Wakurdi wa Syria. Hata hivyo kuendelea operesheni za jeshi hilo la Uturuki katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu, kumeibua ukweli huu kwamba watawala wa serikali ya Ankara wanafanya kila njama kwa ajili ya kuwaokoa magaidi wenye mfungamano na mirengo tofauti ya kijeshi. Katika miezi ya hivi karibuni viongozi wa Uturuki wamefanya kila juhudi kuwaokoa magaidi wenye kufungamana na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Jab'hatu Nusra na hata Daesh (ISIS). Kiasi kwamba ili kufikia lengo hilo, hata wameingia vitani na washirika wao kuhusu masuala ya Syria. Habari za uhakika za hivi karibuni zinaeleza kwamba jeshi la Uturuki sambamba na kuwapatia mafunzo magaidi, linawatumia baadhi yao nchini Libya na katika maeneo mengine yanayofuatiliwa na viongozi wa Ankara. Pamoja na mambo mengine harakati hizo za jeshi la Uturuki zinabainisha wazi hali ngumu ya mgogoro huo ambao taratibu unatoka katika udhibiti wa baadhi ya serikali zenye majivuno hususan za Uturuki na Marekani. Katika uwanja huo, inaonekana kuwa Uturuki kama mmoja wa waingiliaji wa masuala ya ndani ya Syria, ni kati ya nchi zilizoathirika zaidi katika mzozo huo.

Uvamizi wa Uturuki kaskazini mwa Syria umesababisha mauaji kwa raia wa kawaida

Kuhusiana na suala hilo, Ahmad Al-Qatamin, mchambuzi mashuhuri wa masuala ya kisiasa wa nchini Jordan anasema kwamba: "Ni jambo lisilo na shaka kuwa, mgogoro ambao umeiletea matatizo Marekani na kuitumbukiza katika mashinikizo zaidi, sambamba na kuendelea mzozo wa Syria, matatizo hayo pia yamehamia kwa Uturuki; na huenda yakawa na taathira hasi zaidi kwa serikali ya Ankara." Mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa wa Jordan ameongeza kwa kusema: "Ni jambo lililo mbali kwamba operesheni za jeshi la Uturuki nchini Syria zitamalizika hivi karibuni. Hata marafiki wa serikali ya Ankara wanaamini kwamba vita hivyo huenda vikageuka na kuwa vita vya muda mrefu na hivyo kuitumbukiza Uturuki katika mgogoro usio na mwisho." Kiujumla tunaweza kusema kuwa, shughuli za jeshi la Syria ambalo lilianzisha operesheni zake zaidi ya miezi mitatu iliyopita kwa shabaha ya kusafisha mkoa wa Idlib kutokana na uwepo wa magaidi, zimekuwa zikipingwa vikali na serikali ya Uturuki. Alaa kullihal, jeshi la Uturuki na kwa kisingizio cha kupambana na harakati za kigaidi, limeendelea kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya Syria. Hii ni katika hali ambayo uvamizi wa jeshi hilo huko kaskazini mwa Syria, unalaaniwa vikali na raia, serikali ya Syria na jamii ya kimataifa. Pamoja na kuwepo upinzani huo, lakini hivi karibuni serikali ya Uturuki sambamba na kushadidisha uvamizi wake wa ardhi ya Syria, imeendeleza operesheni zake  za kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.