Hizbullah: Muqawama umejiandaa kupambana na maadui
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati hiyo ya muqawama daima iko tayari na imejiandaa barabara kukabiliana na chokochoko za maadui.
Sheikh Naim Qassem ameyasema hayo leo Jumanne na kukumbusha kuwa, katika uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon mnamo April 11, 1996, nchi hiyo ya Kiarabu ilipata ushindi mkubwa na kumfanya adui Mzayuni aondoke kwa fedheha, baada ya wanajihadi wa Hizbullah kushirikiana bega kwa bega na jeshi la Lebanon katika mapambano.
Amesema tangu baada ya ushindi huo, haki ya harakati hiyo ya muqawama kutumia makombora dhidi ya maadui iwapo watafanya uvamizi wowote dhidi ya taifa hilo, ilitambuliwa.
Kadhalika Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amepongeza jitihada za harakati hiyo za kulinda taifa la Lebanon mbele ya uhasama wa utawala wa Kizayuni na pia katika masuala ya kitiba na kijamii.
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon iko mstari wa mbele kukabiliana na kuenea kwa virusi hatari vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Maafisa wa Hizbullah wamekuwa wakitekeleza operesheni za kunyunyiza kemikali za kuua virusi vya Corona katika miji na vijiji vya Lebanon na pia kusambaza chakula na vifaa vya kiafya kwa wananchi ambao wametakiwa wabakie majumbani mwao ili kuzuia kuenea ugonjwa huo.