Sudan: Tumeondoa akthari ya askari wetu nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60995-sudan_tumeondoa_akthari_ya_askari_wetu_nchini_yemen
Serikali ya Mpito wa Sudan imetangaza kuwa imewaondoa nchini Yemen aghalabu ya wanajeshi wake waliokuwa wanapigana chini ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 15, 2020 07:55 UTC
  • Sudan: Tumeondoa akthari ya askari wetu nchini Yemen

Serikali ya Mpito wa Sudan imetangaza kuwa imewaondoa nchini Yemen aghalabu ya wanajeshi wake waliokuwa wanapigana chini ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Baraza la Utawala wa Mpito nchini Sudan, Omar Qamaruddin amesema akthari ya wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwa Yemen wamerejea nyumbani na kusisitiza kuwa wachache waliosalia katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu watarejea nchini karibuni hivi.

Vyama vya siasa vya Sudan vimepongeza hatua hiyo ya kurejeshwa nyumbani aghalabu ya askari wa nchi hiyo, lakini vimesema kuwa uamuzi huo umechelewa sana.

Oktoba mwaka jana, jeshi la Sudan lilianza kuondoka hatua kwa hatua nchini Yemen, ambapo askari elfu 10 waliondoka nchini humo katika awamu ya kwanza.

Mamia ya askari wa Sudan wameuawa katika vita hivyo vya niaba nchini Yemen

Wanajeshi mamluki wa Sudan walitumwa nchini Yemen kushirikiana na Saudi Arabia na Imarati katika vita na mashambulizi yanayoendelea kufanywa dhidi ya taifa la Yemen wakati wa utawala wa Jenerali Omar al Bashir aliyeondolewa madarakani tarehe 11 mwezi Aprili mwaka jana. Al Bashir alituma jeshi la Sudan kupigana Yemen mkabala wa kupewa pesa kutoka Saudi Arabia. 

Kuwepo kwa wanajeshi wa Sudan katika vita vya Yemen kunapingwa sana na makundi ya kisiasa na kijamii ya nchi hiyo hasa baada ya mamia miongoni mwao kuuawa wakipigana kwa niaba ya Saudi Arabia.