Uhusiano mzuri wa Iran na Afghanistan katika kivuli cha mawasiliano endelevu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulika masuala ya sheria amesema kuwa, ili kuzuia magendo ya binaadamu na safari haramu, Tehran imetiliana saini makubaliano mapya na serikali ya Afghanistan.
Mohsen Baharvand ameyasema hayo hivi karibuni mwishoni mwa safari ya siku mbili ya ujumbe wa Iran huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan na kubainisha kwamba katika kipindi cha siku mbili, kulifanyika mazungumzo mazuri na viongozi wa serikali ya nchi hiyo jirani. Ameongeza kuwa Iran na Afghanistan zimekubaliana kwamba safari zote kati ya nchi mbili zitafanyika kwa mujibu wa sheria. Inafaa kuashiria kuwa, hivi karibuni baadhi ya raia wa Afghanistan walidai kupitia video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba walinda mpaka wa Iran katika mpaka wa nchi mbili, waliwatesa raia kadhaa wa Afghanistan na kisha kuwatupa mtoni. Kufuatia hali hiyo baadhi ya vyombo vya habari vya kigeni na kwa lengo la kuharibu uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi mbili hizi jirani na za kirafiki, viliyatumia madai hayo kisiasa kwa ajili ya kuharibu jina zuri la Iran. Viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran walifanya mawasiliano endelevu na viongozi wa Afghanistan kufuatia madai hayo ya kutupwa mtoni raia kadhaa wa Afghanistan na walinda mpaka wa Iran sambamba na kuanzisha uchunguzi wa pamoja kuhusu tukio hilo. Safari ya hivi karibuni ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya sheria nchini Afghanistan ilifanyika katika fremu hiyo.
Katika mazungumzo na viongozi wa Afghanistan, Iran sambamba na kuwasilisha ushahidi, ilisisitiza kwamba walinda mpaka wa Iran hawakuwatesa wala kuwatupa mtoni raia wa nchi hiyo jirani. Kuhusiana na suala hilo Mohsen Baharvand, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria amesisitiza kwamba: "Uchunguzi uliofanywa kuhusiana na kadhia hiyo umebaini kwamba walinda mpaka wa Iran hawakuhusika kwa vyovyote vile na tukio hilo." Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa Iran ina mpaka wa pamoja na Afghanistan wenye urefu wa kilometa 700 ambapo sehemu ya mpaka huo ni nchi kavu na nyingine ikiwa ni ya maji, huwa inakabiliwa na wimbi kubwa la wahajiri haramu. Katika mazingira hayo, suala la kuchukua tahadhari na kuwa macho vyombo vya kulinda mpaka vya Afghanistan ni jambo la dharura ili kwa njia hiyo watu wanaofanya magendo ya binaadamu wasiweze kuathiri uhusiano mwema uliopo kati ya Tehran na Kabul kutokana na ukiukaji sheria wa watu wa namna hiyo. Katika fremu hiyo na kufuatia kujiri mazungumzo ya siku mbili kati ya viongozi wa Afghanistan na Iran, serikali ya Kabul imekubali kwamba vyombo vyake vya kulinda mpaka muda wote vitakuwa macho kwa ajili ya kuzuia safari zisizo za kisheria katika maneo hayo. Uenyeji wa miaka 40 wa Iran kwa wakimbizi wa Afghanistan, unaonyesha kiwango cha ushirikiano mkubwa wa raia wa nchi mbili na pia umuhimu wa uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya Tehran na Kabul.
Aidha kupatiwa bure elimu, nyenzo za maisha na afya hususan katika kipindi cha virusi vya Corona, ni miongoni mwa huduma za kibinaadamu zinazotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wakimbizi wa Afghanistan. Uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kidini na kiutamaduni kati ya Iran na Afghanistan ni wenye histori ndefu. Lugha moja ya Kifarsi, inazidisha uhusiano wa kiudugu kati ya mataifa haya mawili, ambapo madai ya kutupwa mtoni na walinda mpaka wa Iran wahajiri wa Afghanistan, hayawezi kuharibu uhusiano huo mkongwe. Aidha Iran mbali na kuwalinda vizuri wahajiri wa Afghanistan nchini hapa, pia imekuwa ikifuatilia siasa za kuimarisha usalama na uthabiti ndani ya nchi hiyo jirani. Mazungumzo endelevu kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan juu ya udharura wa kuundwa serikali jumuishi nchini humo, yanaonyesha uzingatiaji mkubwa wa Iran juu ya msingi wa kuishi vyema na jirani. Kiujumla ni kwamba miamala mizuri ya Iran kuihusu Afghanistan inatokana na umuhimu wa kuwepo uhusiano mwema na kuzingatiwa majirani. Hii ni kwa kuwa Iran ni mshirika mwenye kuaminika kwa ajili ya Afghanistan ambapo mazungumzo chanya na katika mazingira magumu huweza kuzuia taathira mbaya ya madai yasiyo na msingi yanayokusudia kuharibu uhusiano wa nchi mbili.