Umoja wa Mataifa: Yemen inakabiria kukumbwa na wimbi jingine la njaa
Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen ametahadharisha kwamba, nchi hiyo inakaribia kukumbwa na baa jingine la njaa kutokana na kupungua mno bajeti ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya nchi hiyo.
Bi Lise Grande amesema kuwa, Yemen ambayo kwa miaka sita sasa imekuwa katika vita inakabiliwa na hali mbaya mno ya kibinadamu na huenda ikakumbwa na janga jingine kubwa la njaa kutokana na kupungua bajeti ya Umoja wa Mataifa kwa nchi hiyo.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, mipango ya kutuma misaada ya kibinadamu nchini Yemen ambayo inajumuisha bidhaa za chakula na vifaa vya tiba imevurugika kutokana na hali mbaya ya kiuchumi ulimwenguni ambayo imesababishwa na janga la Corona.
Aidha amesema kuwa, Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilikuwa likiwasaidia Wayameni milioni 13, lakini hivi sasa msaada kwa raia hao umepungua na ni Wayemeni milioni 8.7 tu ndio wanaosaidiwa kwa sasa.
Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Juni Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, zaidi ya Wayameni milioni 20 wanataabika kwa njaa na uhaba mkubwa wa chakula.
Ripoti mbalimbali za mashirika ya misaada ya kibinadamu zinasema kuwa, asilimia kubwa ya wananchi wa Yemen wana uwezo wa kula mlo mmoja tu kwa siku mbili na kwamba, idadi ya watoto wanaotaabika kwa utapiamlo nchini humo ambao umesababishwa na lishe duni imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku.