May 02, 2016 04:03 UTC
  • Umoja wa Mataifa: 741 waliuawa mwezi Aprili nchini Iraq

Takwimu za hivi punde za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa idadi ya watu waliouawa katika machafuko na wimbi la mashambulizi ya kigaidi nchini Iraq mwezi uliopita wa Aprili ni watu 741.

Katika ripoti yake ya kila mwezi iliyotolewa jana Jumapili, UN imesema waliouawa katika kipindi hicho ni raia 410 na maafisa usalama 331. Aidha ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa watu 1,374 wamejeruhiwa katika machafuko hayo mwezi Aprili.

Kadhalika ripoti ya UN imebainisha kuwa, mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad ndio ulioshuhudia idadi kubwa ya vifo katika mwezi huo, ambapo watu 232 waliuawa na wengine 642 kujeruhiwa.

Katika kipindi cha mwezi Machi, watu wasiopungua 1,119 waliuawa katika machafuko nchini Iraq huku idadi ya waliojeruhiwa katika mwezi huo ikipindukia 1,500.

Hii ni katika hali ambayo, makumi ya watu wameuawa katika siku ya kwanza ya mwezi huu wa Mei nchini Iraq. Jana Jumapili, watu zaidi ya 38 waliuawa na wengine 86 kujeruhiwa katika mashambulizi pacha ya mabomu ya kutegwa kwenye magari katika mji wa Samawa, kusini mwa Iraq.

Maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Iraq yamekuwa yakishuhudia wimbi la mashambulizi ya kigaidi kutoka kundi la Daesh, tangu lilipoanzisha hujuma zake za kinyama mwezi Juni mwaka 2014.

Tags