Haaretz: Nasrullah ana taathira na ushawishi usio wa kawaida kwa Waisraeli
Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeandika kuwa, kinachoyafanya maneno ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah yawe na taathira isiyo ya kawaida kwa Wazayuni ni ukweli wake, kutokuwa na mzaha katika kauli zake na uwelewa alionao kwa masuala ya Israel.
Gazeti hilo la Kizayuni limeyaeleza hayo katika toleo lake la jana Jumapili lilipozungumzia taathira ya hotuba na matamshi ya Sayyid Hassan Nasrullah kwa jamii ya Waisraeli.
Kwa mujibu wa Haaretz, Sayyid Hassan Nasrullah alilitimua jeshi la Israel Lebanon na akajenga aina fulani ya kinga ya kutoweza kuhujumiwa nchi hiyo na Israel, kinga na hali ambayo haina mfano wake katika nchi za Kiarabu.
Gazeti hilo la Kizayuni limebainisha kuwa, Waisraeli wanayaamini zaidi maneno anayosema Nasrullah kuliko matamshi yanayotolewa na viongozi wao na hasa kutokana na kauli ya Katibu Mkuu huyo wa Hizbullah kwamba Israel ni dhaifu mno kuliko hata utando wa buibui.
Wakati huohuo utafiti wa kitaalamu uliofanywa na Chuo Kikuu cha Bi'ru-Sab'i kilichoko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) unaonyesha kuwa, Waisraeli wamekatishwa tamaa na viongozi wao na wala hawatokuwa pamoja nao na kuwaunga mkono endapo utawala huo wa Kizayuni utajiingiza kwenye makabiliano yoyote ya kijeshi katika siku za usoni.../