Msimamo wa Sayyid Nasrullah kuhusu mlipuko wa bandari ya Beirut
-
Sayyid Hassan Nasrullah
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah jana usiku alizungumzia mlipuko mkubwa uliotokea katika bandari ya Beirut akisisitiza udharura wa kutambuliwa wahusika wake na kukaribisha misaada ya nchi za kigeni kwa Lebanon.
Jumanne iliyopita mji mkuu wa Lebanon, Beirut ulikumbwa na mlipuko mkubwa ambao umeua zaidi ya watu 150 na kujeruhi wengine karibu elfu tano. Mlipuko huo pia umesababisha hasara kubwa za kiuchumi zinazokadiriwa kufikia mabilioni ya dola za Kimarekani. Hotuba ya jana usiku ya Sayyid Hassan Nasrullah ilikuwa na nukta kadhaa muhimu.
Kwanza ni sisitizo lake kwamba harakati hiyo ya Hizbullah iko tayari kutekeleza majukumu yake ya kitaifa na kibinadamu kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathiriwa na mlipuko huo na kuisitiza udharura wa kuimarishwa mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya kuvuka salama mazingira ya sasa. Sayyid Nasrullah amesema: "Hizbullah iko tayari kushiriki katika operesheni ya kuwapa makazi watu waliopoteza makazi yao katika mlipuko huo."
Nukta ya pili muhimu katika hotuba ya Sayyid Hassan Nasrullah ni hatua yake ya kukaribisha misaada ya kigeni kwa ajili ya kupunguza athari mbaya za mlipuko wa bandari ya Beirut. Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: "Jumbe nyingi kutoka nchi mbalimbali zimewasili Lebanon, na muhimu zaidi ni safari ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mjini Beirut. Hizbullah inaziangalia safari na misaada hiyo kwa mtazamo chanya hasa iwapo misaada na safari hizo zitafanyika katika fremu ya wito wa kuwepo umoja na ushirikiano baina ya makundi mbalimbali." Matamshi hayo ya Sayyid Nasrullah yamebatilisha madai ya mirengo ya kisiasa inayoipakazia Hizbullah kuwa inazuia ushirikiano wa Lebanon na nchi nyingine duniani.
Nukta ya tatu muhimu ni jibu madhubuti la Katibu Mkuu wa Hizbullah dhidi ya madai kwamba, harakati hiyo imehusika na mlipuko wa bandari ya Beirut. Baada ya mlipuko huo wa Jumanne iliyopita, baadhi ya vyombo vya habari vya kigeni hususan vile vinavyomilikiwa au kufadhiliwa na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia vilidai kwamba kulikuwepo maghala ya silaha ya Hizbullah katika bandari hiyo na kwamba maghala hayo ndiyo sababu ya mlipuko huo.
Madai haya pia yamekejeliwa na watumia wa mitandao ya kijamii katika ulimwengu wa Kiarabu. Katika hotuba yake ya jana usiku, Sayyid Nasrullah alisema: “Madai kwamba mlipuko wa Beirut umetokana na maghala ya silaha na makombora ya Hizbullah ni kilele cha dhulma na uhaini dhidi ya harakati hii. Tunakadhibisha kwa nguvu zote madai ya kuwepo aina yoyote ya makombora au mada za milipuko za Hizbullah katika bandari ya Beirut, si katika siku zilizopita wala hivi sasa.”
Nukta ya nne muhimu katika hotuba ya Sayyid Nasrullah ni udharura wa kudumisha tishio dhidi ya utawala haramu wa Israel. Katika wiki za karibuni na baada ya kuuawa shahidi mpiganaji mmoja wa Hizbullah mjini Damascus, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa na woga na wahka mkubwa wa kukabiliwa na jibu kali la Hizbullah. Utawala huo unadhani kwamba, mlipuko wa Beirut na mazingira ya sasa vitapunguza tishio la Hizbullah. Hata hivyo Sayyid Hassan Nasrullah alisema katika hotuba yake ya jana usiku kwamba: “Hizbullah haihusiki na masuala ya bandari ya Beirut wala haidhibiti na kusimamia eneo hilo, na haijui ni vitu gani vilivyoko katika bandari hiyo. Hizbullah inajua zaidi yaliyoko katika bandari ya Haifa kuliko vilivyoko katika bandari ya Beirut. Usimamizi wa bandari ya Beirut si jukumu la Hizbullah, kinyume chake, ina wajibu wa kufuatilia masuala ya bandari ya Haifa; kwa sababu bandari hiyo ni sehemu ya stratijia ya ulinzi ya Lebanon.“
Nukta muhimu ya tano katika hotuba ya Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon ni uungaji mkono wake kwa uchunguzi wa sababu za mlipuko wa bandari ya Beirut na kuwashughulikia watu waliohusika na mlipuko huo. Hata hivyo Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kuwa, uchunguzi huo unapaswa kufanywa na Walebanon wenyewe na anetoa pendekezo kuwa jeshi la Lebanon lifuatilie kadhia hiyo. Kwa pendekezo hilo, Katibu Mkuu wa Hizbullah amebatilisha madai ya kuwepo mgongano kati ya harakati hiyo na jeshi la Lebanon.