Sudan yakanusha taarifa kuhusu mazungumzo na Israel
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imekanusha kauli aliyoitoa msemaji wake kuhusu mawasiliano kati ya Sudan na utawala bandia wa Israel kwa ajili ya kusaini makubaliano ya amani.
Kaimu waziri wa mambo ya nje wa Sudan Omer Gamar-Eddin amesema kupitia taarifa kuwa wizara yake haikujadili uhusiano na Israel. Aidha amesema msemaji wa wizara hiyo Haidar Badawi al-Sadiq hajapewa idhini ya kutoa kauli yoyote kuhusu suala hilo.
Kauli hiyo imekuja huku Umoja wa Falme za Kiarabu ukiendelea kukosolewa vikali kutokana na hatua yake ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kurahisisha uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida kati ya Imarati na utawala haramu wa Kizayuni, Alkhamisi iliyopita pande mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.
Makubaliano hayo kati ya Israel na Imarati yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa duniani, ambao karibu wote wamesisitiza kwa kauli moja kuwa, hatua hiyo ya Imarati ni uhaini na usaliti kwa malengo matukufu ya Palestina.