Imran Khan: Pakistan kamwe haitautambua rasmi utawala haramu wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62903-imran_khan_pakistan_kamwe_haitautambua_rasmi_utawala_haramu_wa_israel
Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kuwa nchi yake kamwe haitautambua rasmi utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 19, 2020 05:26 UTC
  • Imran Khan
    Imran Khan

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kuwa nchi yake kamwe haitautambua rasmi utawala haramu wa Israel.

Imran Khan ameyasema hayo katika mahojiano yake na televisheni ya Dunia News akieleza msimamo wa Pakistan kuhusu hatua ya Imarati ya kukubali kuanzisaha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel. 

Amesema msimamo huo unaoana na agizo lililotolewa na mwasisi wa Pakistan, Muhammad Ali Jinnah wa kulitetea taifa la Palestina mkabala wa utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Waziri Mkuu wa Pakistan amesisitiza kuwa Islamabad kamwe haitaitambua rasmi Israel maadamu utawala huo bado unaikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Amesema Waislamu wanapaswa kuwajibika mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na kadhia ya Palestina.

Alhamisi iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza habari ya kufikiwa mapatano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili. Hatua hiyo imelaaniwa na harakati zote za mapambano ya ukombozi wa Palestina. 

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amelaani hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: Hatua hiyo ya Imarati ni kosa kubwa na usaliti kwa malengo ya Wapalestina na Quds tukufu.