Kufanya safari tena Rais wa Ufaransa nchini Lebanon
Baada ya kupita takriban mwezi mmoja tangu kutokea mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa mara ya pili ameelekea nchini Lebanon.
Macron amesema lengo la safari yake hiyo ni kutathmini matukio yanayohusiana na misaada ya haraka na ushirikiano wa pamoja wenye lengo la kuandaa mazingira ya lazima kwa minajili ya kufanya ukarabati na uthabiti katika mji mkuu Beirut. Hii ni safari ya pili ya Rais huyo wa Ufaransa nchini Lebanon baada ya mlipuko wa Beirut wa Agosti 4.
Moto uliotokea katika mojawapo ya maghala ya bandari ya Beirut ulisababisha mlipuko mkubwa katika maghala mengine jirani yaliyokuwa na tani 2,700 mada za amoniamu naitreti. Zaidi ya watu 190 waliaga dunia katika mlupuko huo na wengine karibu elfu sita kujeruhiwa.
Kufuatia mlipuko huo, anga ya kisiasa na kiuchumi ya Lebanon ambayo kimsingi ilikuwa na kiwingu ikazidi kuwa mbaya zaidi. Ukweli wa mambo ni kuwa mlipuko wa Beirut ulichukua mkondo wa kisiasa zaidi na kuwapatia kisingizio kizuri wapinzani wa serikali ambapo walianza kufanya mikusanyiko mikubwa wakilalamikia sera za serikali na jinsi ilivyoshindwa kukabiliana na umasikini na hali mbaya ya kiuchumi.

Sauti ya wapinzani ilimfanya Rais Michel Aoun wa nchi hiyo azungumzie suala la kuweko mgogoro ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo. Rais Aoun alisema: Hii leo Lebanon inakabiliwa na mgogoro ambao haujawahi kushuhudiwa na miongo kadhaa ya mrundikano wa migogoro ya kisiasa, kiuchumi, fedha na maisha ya wananchi umefikia hatua ya kulipuka, na wananchi wa Lebanon wanataka mabadiliko katika muundo wa nchi, hivyo ni lazima kuheshimu matakwa ya wananchi na bila shaka muda wa mageuzi umewadia.
Katika upande mwingine, mlipuko huo mkubwa wa Beirut ulifungua njia ya madola ya kigeni kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo, ambapo katika siku ya tatu baada ya mlipuko huo, Rais Emmanuel Macron alielekea katika nchi hiyo ya Kiarabu. Macron alielekea Lebanon akiwa amejivika vazi la mtoaji misaada ya kibinadamu na ahadi za kuisaidia nchi hiyo ambapo akiwa nchini humo alitoa matamshi ya uingiliaji masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa kutaka kufanyika mageuzi katika muundo wa kisiasa wa Lebanon. Hata ahadi yake ya msaada ilifungamana na sharti hilo.
Macron mara hii ameelekea Lebanon katika hali ambayo, matamshi yake ya mwezi mmoja uliopita alipokuwa Beirut, yalikabiliwa na ukosoaji mkubwa wa weledi wa mambo ndani ya Lebanon ambao sambamba na kusisitiza kuwa, mamlaka ya usimamizi wa Ufaransa kwa nchi hiyo yalifikia tamati 1943.
Safari na msimamo huo wa Rais Macron ni juhudi za kutaka kuweko tena Ufaransa katika uga wa siasa za ndani za Lebanon.

Kuhusiana na jambo hilo, Dima Swadiq, mwandishi habari wa Kilebanon ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Ishara za ombwe la uongozi na kutopata mafanikio mfumo unaotawala nchini Lebanon ndio mambo yaliyomskuma Rais wa nchi ambayo Lebanon ilijikomboa kutoka katika makucha yake mwaka 1960 ajitokeze na kutoa matamshi kama hayo.
Macron alikamilisha safari yake ya awali nchini Lebanon na kurejea nchini kwake ambapo alitangaza kuwa, anataka kuweko mageuzi na kufanyika uchaguzi wa mapema nchini Lebanon.
Hivi sasa Macron ameelekea nchini Lebanon katika safari yake ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja akieleza kuwa, lengo la safari yake ni kutathmini matukio yanayohusiana na misaada ya haraka na ushirikiano wa pamoja wenye lengo la kuandaa mazingira ya lazima kwa minajili ya kufanya ukarabati na kurejesha uthabiti katika mji mkuu Beirut.
Hata hivyo safari ya Macron huko Beirut inafanyika katika hali ambayo, Lebanon inaendelea kushuhudia matukio ya ndani ya kisiasa. Baada ya kujiuzulu serikali ya Waziri Mkuu Hassan Diab akiitikia wito wa wananchi kutokuwa na utendaji mzuri serikali yake, hivi sasa Mustapha Adib amepewa jukumu la kuunda serikali mpya ya nchi hiyo.

Inaonekana kuwa, hivi sasa vyama vyote vya siasa nchini Lebanon vimefikia natija hii kwamba, katika mazingira ya sasa ya mgogoro, kuna ulazima wa kufanyika mageuzi ya kisiasa sambamba na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa ajili ya kuiokoa nchi hiyo na mazingira ya sasa. Katika upande mwingine, mirengo ya kisiasa nchini Lebanon licha ya kuwa inataka kuweko ushirikiano wa kimataifa katika kukarabati na kuboresha muundo wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo, lakini inapinga vikali uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao.
Gebran Bassil, Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon sanjari na kuashiria kwamba, uingiliaji wa ajinabi katika masuala ya ndani ya Lebanon siyo tu kwamba, hauleti na kuimarisha uthabiti wa nchi hiyo, bali uingiliaji wa hivi karibuni umeifanya nchi hiyo irejee nyuma katika kipindi cha kabla ya mwaka 1920 amesema: Kuzingirwa Lebanon kutoka nje, kumepelekea kusambaratika uchumi wa nchi. Madola ya Magharibi kwa miaka kadhaa sasa yameiwekea Lebanon mashinikizo ambayo lengo lake hasa ni kuidhoofisha harakati ya muqawama nchini humo.
Hivi sasa Lebanon inapitia kipindi cha mgogoro. Ufaransa kwa sura ya wazi na madola mengine ya Magharibi na ya Kiarabu hususan Marekani yanafuatilia kwa umakini mkubwa matukio ya Lebanon. Pamoja na hayo inaonekana kuwa, mstari mwekundu wa Walebanon ni kutokubali uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao. Kama aivyosisitiza Gebran Bassil aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon ni kuwa: Tusaidieni ili tuyashajiishe madola makubwa ya kieneo na kimataifa yasiibadilishe Lebanon na kuifanya kuwa uwanja na medani ya vita na mapigano.