May 03, 2016 16:30 UTC
  • Magaidi waendeleza ukatili Syria, makumi wauawa Aleppo

Makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi za kigeni yameshambulia hospitali na maeneo kadhaa ambayo yako chini ya udhibiti wa serikali katika mji wa Aleppo, kaskazini mwa Syria na kusababisha mauaji ya watu wasiopungua 19.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limesema kwa akali wanawake 3 wameuawa na wengine 17 kujeruhiwa baada ya magaidi hao kushambulia kwa maroketi Hospitali ya al-Dabit, katika eneo linalodhibitiwa na serikali la Muhafaza. Aidha watu wengine 11 wameuawa baada ya magaidi hao kushambulia maeneo ambayo yako chini ya udhibiti wa serikali katika mji huo.

Shirika la kutetea haki za binadamu linalojulikana kama Syrian Observatory for Human Rights lenye makao makuu yake nchini Uingereza limedai kuwa waliouawa katika hujuma za magaidi hao mjini Aleppo hii leo ni watu 19.

Taarifa ya jeshi la Syria imesema kuwa kundi la kigaidi la al-Nusra lenye mafungamano na mtandao wa al-Qaeda, kundi la Ahrar al-Sham na Jaish al-Islam ndiyo yaliyohusika na mashambulio ya leo Jumanne.

Ijumaa iliyopita magaidi wa kitakfiri wa Daesh walilenga eneo lililoko kando na msikiti wa Malakhan katika medani ya 'Babul-Faraj' na makazi ya raia katika mji wa Aleppo kaskazini mwa nchi ambapo zaidi ya watu 33 waliuawa na zaidi ya wengine 165 kujeruhiwa.

Tags