Viongozi wawili wakuu wa Daesh watiwa mbaroni kaskazini mwa Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64021-viongozi_wawili_wakuu_wa_daesh_watiwa_mbaroni_kaskazini_mwa_iraq
Vyombo vya usalama vya Iraq vimetangaza taarifa ya kutiwa mbaroni makamanda wawili wakuu wa kundi la kigaidi la Daesh katika mikoa ya Kirkuk na Salahuddin.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2020 00:55 UTC
  • Viongozi wawili wakuu wa Daesh watiwa mbaroni kaskazini mwa Iraq

Vyombo vya usalama vya Iraq vimetangaza taarifa ya kutiwa mbaroni makamanda wawili wakuu wa kundi la kigaidi la Daesh katika mikoa ya Kirkuk na Salahuddin.

Kitengo cha habari cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq jana kilitangaza kuwa maajenti wa wa kitengo hicho wamefanikiwa kumtia mbaroni kiongozi mmoja wa Daesh katika oparesheni ya pamoja waliyofanya na idara ya usalama ya mkoa wa Kirkuk.   

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq imeongeza kuwa, kutiwa mbaroni kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Daesh kumejiri baada ya kuundwa timu maalumu na kufuatia kufuatiliwa gaidi huyo wa Daesh kwa zaidi ya mwezi mmoja. Katika uchunguzi wa awali gaidi huyo amekiri kuwa ni mwanachama wa kundi la kigaidi la Daesh na kushiriki kwenye oparesheni kadhaa za kigaidi, vitendo vya utekaji nyara na kuwaua raia wa Iraq.  

Yahya Rasul Msemaji wa Kamandi Kuu ya vikosi vya ulinzi vya Iraq pia ametangaza habari ya kutiwa mbaroni gaidi mwingine wa Daesh katika mkoa wa Salahuddin nchini humo.  

Yayha Rasul, Msemaji wa Kamandi Kuu ya vikosi vya ulinzi vya Iraq

Masalia ya wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh wangali wapo katika maeneo mbalimbali ya Iraq na wanaendelea kufanya oparesheni za kigaidi licha ya kundi hilo kupata kipigo kikali nchini humo.