Ujenzi haramu wa vitongoji Palestina umeongezeka maradufu katika utawala wa Trump
Kundi liitwalo "Amani Sasa" lililoko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la Israel limetangaza kuwa, ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina katika kipindi cha miaka minne ya urais wa Donald Trump nchini Marekani umeongezeka maradufu.
Kundi hilo la Amani Sasa ambalo linafuatilia ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala haramu wa Israel katika ardhi za Wapalestina limetoa ripoti maalumu kuhusiana na suala hilo na kutangaza kuwa, katika kipindi hicho cha miaka minne na kwa msaada wa Washington,Tel Aviv imefanya juu chini kuhakikisha inatekeleza mpango wa kuzimega sehemu zingine za Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi unazozikalia kwa mabavu hivi sasa kwa kutumia mbinu hiyo ya ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya mwaka 2017 hadi 2020 iliafikiwa kujengwa nyumba 26,331 katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, wakati katika kipindi cha kati ya mwaka 2013 hadi 2016 idadi ya nyumba zilizoamuliwa kujengwa ilikuwa ni 10,331.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, katika mwaka huu wa 2020, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umebomoa majengo yapatayo 689 katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Baitul Muqaddas na kusababisha Wapalestina 869 wabaki bila makazi.../