Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa: Israel ni dola vamizi
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio linaloutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni dola vamizi na ghasibu.
Kamati ya Pili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Jumatano ilipasisha azimio ambalo limeitaja Israel kuwa ni dola ghasibu na kusisitiza kuwa, mabadiliko ya aina yoyote yaliyofanywa kwenye mipaka ya mwaka 1967 katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina, hayakubaliki.
Azimio hilo limepasishwa kwa kura 153 za ndio na kupingwa na kura 6. Nchi nyingine 16 hazikupiga kura.
Azimio la Baraza Kuu la UN pia limeeleza wasiwasi wake kutokana na operesheni ya Israel ya kuendelea kuharibu sehemu kubwa ya mashamba na ardhi ya kilimo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo, na vilevile ubomoaji wa miundombinu ya kiraia kama mitandao ya maji na vituo vya umeme.
Nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia zimetahadharisha kuhusu athari mbaya za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina ambao unavuruga haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi na kijamii za watu wa Palestina katika ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu ikiweno Quds tukufu,
Ni vyema kukumbusha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kukikua maazimio na sheria za kimataifa kwa kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina kutokana na himaya ya Marekani.