Hizbullah yalaani mauaji ya mkosoaji wa harakati hiyo ya Lebanon
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali mauaji ya mwanaharakati wa kisiasa na mtafiti wa nchi hiyo ya Kiarabu, Lokman Slim aliyeuawa katika mazingira ya kutatanisha.
Taarifa ya Hizbullah imevitaka vyombo vya usalama na mahakama vya nchi hiyo kuchunguza mauaji hayo na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa ukatili huo.
Hizbullah imeonya juu ya kutumiwa kisiasa mauaji hayo na maadui wa ndani na nje ya nchi hiyo ya Kiarabu. Kadhalika harakati hiyo ya muqawama imetoa indhari kwa vyombo vya habari kutumia vibaya mauaji hayo kwa madhara ya usalama na uthabiti wa nchi hiyo.
Mwili wa Slim ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Hizbullah ulipatikana mapema jana Alkhamisi ndani ya gari lake katika kijiji cha Addoussieh, kusini mwa nchi ukiwa na majeraha ya risasi.
Mauaji ya kutatanisha ya mwanaharakati huyo wa kisiasa yameibua wasi wasi wa kuongezeka taharuki ya kisiasa nchini Lebanon.
Mauaji ya namna hii ya wanaharakati wa kisiasa wanaotajwa kuwa wakosoaji wa Hizbullah yamekuwa yakifanyika nchini Lebanon kwa shabaha ya kutaka kulichafua jina la harakati hiyo ya mapambano.