Wapalestina waandamana Ukanda wa Gaza kulaani mzingiro wa Israel
(last modified Sun, 08 May 2016 13:07:58 GMT )
May 08, 2016 13:07 UTC
  • Wapalestina waandamana Ukanda wa Gaza kulaani mzingiro wa Israel

Mamia ya wananchi wa Palestina wameingia mabarabarani kufanya maandamano ya kulaani mzingiro wa kibaguzi wa takriban mwongo mmoja uliowekwa na Utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba picha za watoto watatu waliopoteza maisha jana baada ya nyumba yao kuteketea katika kambi ya wakimbizi ya al-Shati katika Ukanda wa Gaza. Mkasa huo wa moto uliripotiwa kusababishwa na mshumaa ikizingatiwa kuwa umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara katika ukanda huo na haswa eneo la Ramallah.

Hii ni katika hali ambayo, askari wa Utawala haramu wa Israel wameanzisha chokochoko mpya dhidi ya Wapalestina wa Gaza. Siku ya Jumatano, askari wa Utawala haramu wa Kizayuni walishambulia maeneo ya mpakani mwa Ukanda wa Gaza ambapo katika kujibu hujuma hiyo, wanamuqawama wa Palestina walipambana na askari hao.

Mashambulio yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza ni ukiukaji wa makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa baina ya pande mbili mwezi Agosti mwaka 2014 baada ya vita vya siku 50, ambapo Utawala haramu wa Israel uliwaua shahidi zaidi ya Wapalestina 2,300 wakiwemo wanawake na watoto na kuwajeruhi maelfu ya wengine. Hata hivyo, Ismail Ridhwan, Kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, harakati hiyo itatoa majibu makali dhidi ya wanajeshi wa Utawala wa Kizayuni wanaojipenyeza kwenye Ukanda wa Gaza.