Saudia yaongeza kasi ya kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i67268-saudia_yaongeza_kasi_ya_kutangaza_uhusiano_wa_kawaida_na_wazayuni
Chombo kimoja cha utawala wa Kizayuni wa Israel kimefichua kuwa viongozi wa Saudi Arabia wameongeza kasi ya kuharakisha kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kwani wanahofia misimamo ya kisiasa ya serikali ya hivi sasa Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2021 23:21 UTC
  • Saudia yaongeza kasi ya kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni

Chombo kimoja cha utawala wa Kizayuni wa Israel kimefichua kuwa viongozi wa Saudi Arabia wameongeza kasi ya kuharakisha kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kwani wanahofia misimamo ya kisiasa ya serikali ya hivi sasa Marekani.

Kanali ya 11 ya televisheni ya Israel ilitangaza hayo jana (Alkhamisi) na kuongeza kuwa, katika siku za hivi karibuni, mawasiliano yameongezeka baina ya ya viongozi wa ngazi za juu wa Saudia na Israel na kwamba mazungumzo ya pande hizo mbili yamejikita zaidi katika mabadiliko ya kisiasa ya serikali ya hivi sasa ya Joe Biden huko Marekani.

Kabla ya hapo pia kanali ya televisheni ya Israel iitwayo KAN ilifichua habari ya kuzinduliwa nambari maalumu ya mawasiliano baina ya Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya uratibu wa kisiasa wa pande hizo mbili kuhusu misimamo ya serikali mpya ya Marekani.

Damu ya Khashoggi inaendelea kumuandama bin Salman, mrithi wa kiti cha Saudia 

 

Kanali ya 11 ya televisheni ya Israel pia imeripoti kuwa, woga mkubwa walio nao viongozi wa Saudia ni msimamo wa serikali ya Joe Biden kuhusu haki za binadamu nchini humo na kufuatiliwa mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi Msaudia aliyekuwa anawakosoa watawala wa kiimla wa nchi hiyo. Watawala wa Saudia ambao hawapendi hata kidogo kukosolewa, walimuua kinyama mwandishi huyo na mwili wake kuukata vipande vipande ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki.

Hiyo ilikuwa ni kashfa kubwa iliyoutikisa ulimwengu. Hata hivyo rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alitumia nguvu zake zote kuwaunga mkono viongozi wa Saudia na kulizima angalau kwa muda suala hilo. Sasa hivi viongozi wapya wa Marekani wamelifufua jambo hilo, suala ambalo limezidi kuwatia kihoro viongozi wa Saudia.