Ansarullah: Marekani haitaki amani irejee Yemen
Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema: Serikali ya Marekani kwa matamshi yake ya upotoshaji na yasiyo ya kimantiki imeonyesha kuwa haitaki kuona amani ikirejea Yemen."
Mohammad Abdulsalam, Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ameongeza kuwa, haiwezekani kutoa nara na kauli mbio za ubinadamu na kubainisha wasi wasi kuhusu hali mbaya iliyoko Yemen kutokana na mzingiro na vita na kisha wakati huo huo kuendelea kuwauzia wavamizi silaha.
Abdulsalam amesema Marekani inafahamu vyema kile ambacho kitapelekea amani kurejea Yemen. Ameongeza kuwa Marekani inapaswa kuwalazimu wavamizi wa Yemen wasitishe vita na mzingiro wao dhidi ya nchi hiyo ili jitihada za kidiplomasia za kusaka amani ziweze kuzaa matunda.
Kauli hiyo ya Abdulsalam imekuja baada ya Ofisi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuwasiliana na Martin Griffiths, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen na kubainisha wasiwasi kuhusu hali ya kibinadamu Yemen.
Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani.
Moto wa vita uliowashwa na Saudia na washirika wake dhidi ya Yemen umeshasababisha maelfu ya Wayemeni kuuawa, makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kupoteza makazi yao na kuwa wakimbizi.