‘Israel inashirikiana na magaidi katika hujuma zake dhidi ya Syria’
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i68048-israel_inashirikiana_na_magaidi_katika_hujuma_zake_dhidi_ya_syria’
Serikali ya Syria imesema utawala wa Kizayuni wa Israel unashirikiana na magaidi katika hujuma zake dhidi ya Syria.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Mar 18, 2021 23:15 UTC
  • ‘Israel inashirikiana na magaidi katika hujuma zake dhidi ya Syria’

Serikali ya Syria imesema utawala wa Kizayuni wa Israel unashirikiana na magaidi katika hujuma zake dhidi ya Syria.

Katika barua ya malalamiko kwa Umoja wa Mataifa, Syria imesema hujuma ya hivi karibuni ya angani yaliyofanywa na Israel dhidi ya Syria, imejiri sambamba na mashambulizi ya magaidi dhidi ya askari wa Jeshi la Syria. Kwa msingi huo ni wazi kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukishirikiana na magaidi kabla ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya Syria, imesema barua hiyo ya malalamiko iliyowasilishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria.

Aidha Syria imesema utawala wa Kizayuni wa Israel mbali na kushirikiana na magaidi pia unashirikiana na makundi yanayotaka kujitenga na nchi hiyo kwa lengo la kuurefusha zaidi mgogoro wa Syria.

Jumanne shirika rasmi la habari la Syria SANA lilitangaza kuwa jeshi la anga la nchi hiyo likikabiliana na makombora kadhaa ya utawala wa Israel ambayo yalikuwa yanavurumishwa kutoka upande wa Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu kuelekea maeneo yanayouzunguka mji mkuu, Damascus.

Magaidi Syria wanaopata himaya ya Israel

Aidha Jumanne pia magaidi wanaopata himaya ya kigeni waliwaua wanajeshi kadhaa wa Syria baada ya kushambulia basi lao kaitka eneo la Dara’a. Jeshi la Syria pia limetangaza kuzima njama ya hujuma kubwa ya kigaidi iliyokuwa inapangwa kutekelezwa mjini Damascus.

Mashambulizi hayo yaliyo kinyume cha sheria ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria yamefanyika katika hali ambayo makundi ya kigaidi Syria yamedhoofika. Kwa msingi huo mashambulizi hayo yanalenga kusaidia makundi ya kigaidi na kuyapa motisha wa kupambana na Jeshi la Syria na waitifaki wake.