Baraza la Usalama latakiwa kuwalaani watenda jinai badala ya kuwashukuru
Mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen amelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, baraza hilo badala ya kuwashukuru magaidi wanaolitendea jinai taifa la Yemen linapaswa kuwalaani.
Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema hayo katika ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa twitter na kueleza kwamba, kikao cha leo cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa badala ya kulaani mzingiro unaendelea kufanywa na watenda jinai dhidi ya taifa la Yemen, kitawashukuru watenda jinai hao.
Muhammad Ali al-Houthi ameongeza kuwa, kikao chochote kile ambacho hakihitimishi mgogoro mbaya kabisa wa kibinadamu na hakiwatambui kuwa ni wahalifu wahusika wa ugaidi huu hakina faida yoyote.
Kabla ya hapo pia, Muhammad Ali al-Houthi alinukuliwa akisema kuwa, siku hizi jumuiya za kimataifa, badala ya kuzilaani nchi mahasimu wa taifa la Yemen kama Marekani, Uingereza, Saudi Arabia na Imarati zinazowaua raia wa Yemen na kulizingira taifa hilo, zinazishukuru nchi hizo wakati zinapofanya jambo dogo sana kama kwa mfano kuruhusu meli kutia nanga katika bandari za Yemen.
Mwezi Machi 2015, utawala wa Saudi Arabia ukiungwa mkono na Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na nchi zingine kadhaa uliivamia kijeshi nchi masikini ya Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani ambao unaendelea hadi sasa.