Mkutano wa amani ya Afghanistan uliopangwa kufanyika Uturuki waakhirishwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i69284-mkutano_wa_amani_ya_afghanistan_uliopangwa_kufanyika_uturuki_waakhirishwa
Mkutano wa amani ya Afghanistan ambao ulipangwa kufanyika mjini Istanbul Uturuki umeakhirishwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2021 07:04 UTC
  • Mkutano wa amani ya Afghanistan uliopangwa kufanyika Uturuki waakhirishwa

Mkutano wa amani ya Afghanistan ambao ulipangwa kufanyika mjini Istanbul Uturuki umeakhirishwa.

Mkutano huo uliokuwa umepangwa kuanza kufanyika tarehe 24 ya mwezi huu wa Aprili huko Istanbul umeakhirishwa na kwamba, sasa utafanyika baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Afisa mmoja wa serikali ya Afghanistan amedokeza kuwa, mkutano huo wa Istanbul umeakhirishwa baada ya kundi la wanamgambo wa Taliban kutangaza kuwa halitashiriki kongamano hilo.

Zabiullah Mujahid, msemaji wa kundi la wanamgambo wa Taliban amenukuliwa na duru za habari akisema kuwa, madhali vikosi vya kigeni vingalipo katika ardhi ya Afghanistan, kundi hilo halitashiriki mkutano wowote ule ukiwemo huu wa Istanbul Uturuki ambao umesogezwa mbele.

Moja ya mazungumzo ya amani ya wanamgambo wa Taliban na serikali

 

Msemaji huyo wa wanamgambo wa Taliban ameeleza kwamba, baadhi ya mataifa yanataka kuingilia masuala ya ndani ya Afghanistan kupitia kongamano la Istanbul.

Zabiullah Mujahid amesisitiza kuwa, wananchi wa Afghanistan wana haki ya kujiamulia mambo yao wao wenyewe bila ya kuingiliwa na mtu mwingine.

Hivi karibuni Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan aliashiria uamuzi uliotangazwa hivi karibuni na Rais wa Marekani Joe Biden wa kuwaondoa askari wa jeshi la nchi hiyo walioko nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa, taifa hilo kamwe halitaporomoko kwa sababu ya kuondoka wanajeshi hao vamizi.