Amnesty International: Waasi wa Syria wametenda jinai za kivita
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kuwa, makundi yanayobeba silaha nchini Syria yametenda jinai za kivita.
Taarifa ya Amnesty International imeeleza kupitia taarifa kwamba, makundi yanayobeba silaha yaliyoko kando ya eneo la Sheikh Maqsood katika mji wa Halab mara kadhaa yamefanya mashambulio ya kiholela dhidi ya makazi ya raia, barabarani, kwenye masoko na misikiti ya Wakurdi katika eneo hilo na kupelekea makumi ya raia kuuawa na kujeruhiwa.
Aidha imeelezwa katika taarifa hiyo ya Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International kwamba, mashambulio hayo yanaweza kuwa ni utendaji wa jinai za kivita kutokana na kutoheshimu maisha ya raia wakati wa kufanyika kwake.
Wakati huo huo makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya kigeni huko Syria yamewaua raia 19 katika kitongoji kimoja katikati mwa nchi hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, waliouawa na magaidi hao katika kijiji hicho ni Maalawi ambao ni kabila la wachache katika kijiji hicho kilichoko katika mkoa wa Homs.
Raia wengine kadhaa wamechukuliwa mateka na kundi hilo la kigaidi linalojiita 'haki za Binadamu Syria.'
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 baada ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani na waitifaki wake kuanzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya raia na maafisa wa serikali ya Syria kwa nia ya kutaka kuipindua serikali halali ya Rais Bashar al Assad wa nchi hiyo.