Nasrullah: Kuteka tovuti za muqawama kumefichua unafiki wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71690-nasrullah_kuteka_tovuti_za_muqawama_kumefichua_unafiki_wa_marekani
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kitendo cha Marekani cha kuteka na kufunga tovuti kadhaa za vyombo vya habari vya kambi ya muqawama kimedhihirisha unafiki wa Marekani inayodai kuwa mtetezi mkubwa wa demokrasia na uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 26, 2021 08:05 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah
    Sayyid Hassan Nasrullah

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kitendo cha Marekani cha kuteka na kufunga tovuti kadhaa za vyombo vya habari vya kambi ya muqawama kimedhihirisha unafiki wa Marekani inayodai kuwa mtetezi mkubwa wa demokrasia na uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari.

Sayyid Hassan Nasrullah alisema hayo jana Ijumaa katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni na kufafanua kuwa, hatua ya Marekani ya kufunga tovuti hizo za habari imeanika hadaa ya Marekani kwa walimwengu kwamba inapigania demokrasia duniani na uhuru wa kujieleza.

Amesema tovuti hizo za habari za mrengo wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi zimefungwa kutokana na nafasi yao muhimu katika kuunga mkono kadhia ya Palestina, mkabala wa ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel.

Sayyid Nasrullah amebainisha kuwa, tovuti hizo za kambi ya mapambano ya Kiislamu zimefungwa kutokana na kusimama kwao kidete dhidi ya ubeberu wa Marekani na magenge ya kigaidi na kitakfiri.

Hujuma ya US dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari

Kabla ya hapo, Mkuu wa Ofisi ya Mahusiano ya Umma ya Hizbullah Mohammad Afif alisema kitendo hicho kiovu cha Marekani kinalenga kuficha ukweli kuhusu jinai ambazo imezitenda pamoja na waitifaki wake dhidi  ya watu wanaodhulumiwa katika eneo hasa watu wa Yemen na Palestina ambao wanakabiliwa na mzingiro mbaya zaidi.

Jumanne iliyopita, Washington iliendeleza sera za kijuba na kibeberu za nchi hiyo kwa kuzifunga tovuti za televisheni za kimataifa za Iran na vyombo vya habari vya mrengo wa muqawama vya Yemen, Palestina, Iraq na Bahrain. Televisheni ya Kiingereza ya Iran ya Press TV na zile za Kiarabu za Al Alam na Al Khauthar ni miongoni mwa vyombo vya habari ambavyo vimefungiwa tovuti zao na Marekani.