May 17, 2016 13:53 UTC
  • Watu 58 wauawa katika mashambulizi ya bomu Baghdad, Iraq

Kwa akali watu 58 wameuawa na wengine zaidi ya 90 wamejeruhiwa katika mashambulizi matatu ya bomu yaliyoutikisa mji mkuu wa Iraq, Baghdad hii leo.

Habari zinasema kuwa, watu 17 wameuawa na wengine 28 kujeruhiwa katika shambulizi la bomu lililolenga soko moja lenye shughuli nyingi katika wilaya ya al-Shaab, kaskazini mwa mji huo. Kadhalika watu sita wameripotiwa kuuawa katika shambulizi la pili la bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari katika mji wa al-Rasheed, kusini mwa nchi, huku watu wengine kadhaa wakipoteza maisha katika hujuma ya tatu iliyotokea katika eneo la Abu Ghraib, magharibi mwa mji mkuu Baghdad. Hata hivyo hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika na mashambulizi hayo ya leo, ingawa hujuma za kikatili za aina hii zimekuwa zikifanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Haya yanajiri siku chache baada ya askari 17 wa jeshi la Iraq kuuawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na matakfiri wa Daesh katika mkoa wa Anbar, magharibi mwa nchi hiyo. Aidha watu wasiopungua 64 waliuawa na wengine zaidi ya 85 kujeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea karibu na soko la Urayda katika kitongoji cha Sadr mashariki mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, Jumatano iliyopita. Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, mgogoro wa kisiasa wa hivi sasa nchini humo uliozushwa na hatua yake ya kutaka kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri kwa lengo la kukabiliana na ufisadi, umefungua mlango wa kushamiri harakati za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini humo.

Tags