Kuhuishwa uhusiano wa Qatar na Misri baada ya Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73956-kuhuishwa_uhusiano_wa_qatar_na_misri_baada_ya_saudi_arabia
Salim Mubarak Al Shafi balozi wa Qatar mjini Cairo Jumatatu wiki hii alikutana na kufanya mazungumzo na Sameh Hassan Shoukry Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na akamkabidhi hati yake ya utambulisho.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 26, 2021 13:45 UTC
  • Kuhuishwa uhusiano wa Qatar na Misri baada ya Saudi Arabia

Salim Mubarak Al Shafi balozi wa Qatar mjini Cairo Jumatatu wiki hii alikutana na kufanya mazungumzo na Sameh Hassan Shoukry Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na akamkabidhi hati yake ya utambulisho.

Katika miaka ya karibuni uhusiano wa Qatar na Misri umegubigwa na  mivutano chungu nzima. Qatar iliunga mkono mapinduzi ya wananchi wa Misri hapo mwaka 2011 dhidi ya utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Hosni Mubarak. Doha pia ambayo ilikuwa mwenyeji wa wawakilishi na viongozi wengi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri iliunga mkono kuingia madakarani harakati hiyo nchini Misri. Doha pia ilikitaja kitendo cha wanajeshi wa Misri kutwaa madaraka ya nchi kuwa ni mapinduzi dhidi ya Ikhwanul Muslimin. Msimamo huu wa Qatar kuhusiana na Ikhwanul Muslimin ulikuwa sababu kuu iliyoibua mivutano katika uhusiano wa Doha na Cairo.  

Uungaji mkono wa Qatar kwa Ikhwanul Muslimin ya Misri 

Mwaka 2017 pia Misri ilikuwa moja kati ya nchi 4 za Kiarabu ambazo zilikata uhusiano wao na Qatar. Mwezi Juni mwaka 2017 Saudi Arabia, Misri, Imarati na Bahrain zilichukua uamuzi wa kukata mahusiano na Qatar kwa visingizio chungu nzima; moja ya visingizio hivyo kikitajwa kuwa ni uungaji mkono wa Doha kwa harakati ya Ikhwanul Muslimin. Nchi hizo nne ziliitaja Ikhwanul Muslimin kuwa ni taasisi ya kigaidi na kuituhumu Qatar kuwa inaunga mkono ugaidi.    

Hivi sasa Doha na Cairo zimehuisha uhusiano wao, na mwezi Januari mwaka huu Saudi Arabia ilikuwa mwenyeji wa kikao cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambapo Qatar pia ilialikwa katika kikao hicho. Sheikh Tamim Amir wa Qatar  binafsi alihudhuria mkutano huo uliofanyika katika mji wa Al-'Ula baada ya kususia vikao vya baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu. Hatua hiyo ilihitimisha mivutano iliyokuwepo baina ya nchi yake na Saudia. 

Amir wa Qatar, Sheikh Tamim 

Hatua hiyo ya Saudi Arabia ilikosolewa na kupingwa na Misri kwa sababu serikali ya Cairo iliamini kuwa, Riyadh ilifanya hivyo bila ya kushauriana na nchi nyingine tatu ambazo Juni 2017 zilikata uhusiano wao na Doha. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Samih Shoukry tarehe 15 Juni mwaka huu alifaya safari mjini Doha na kukutana na mwenzake wa Qatar, Muhammad bin Abdulrahman Aal Thani. Pande mbili zilijadili suala la kuimarisha ushirikiano na uhusiano. Qatar imemuarifisha balozi wake huko Cairo baada ya kumtuma balozi wake mpya huko Saudia mwezi uliopita. Katika upande mwingine, mwezi Juni mwaka huu Misri pia ilichukua uamuzi wa kumuarifisha Amr Al Sherbini kama balozi wake nchini Qatar. Hatua hii ya kuhuisha uhusiano wa pande mbili imejiri katika hali ambayo Qatar haijatekeleza hata sharti moja kati ya masharti 13 iliyoainishiwa na nchi nne za Kiarabu kwa ajili ya kurejesha uhusiano wao na Doha. Pamoja na hayo, kuanzishwa uhusiano baina ya Doha, Riyadh na Cairo kunaashiria nukta mbili muhimu.  

Samih Shoukry, Wazri wa Mambo ya Nje wa Misri ambaye Juni mwaka huu alifanya ziara mjini Doha 

Ya kwanza ni kuwa, Qatar inatilia mkazo suala la kustawisha ushirikiano na uhusiano na nchi za Kiarabu na haipendezwi wala kukaribisha hatua yoyote ya kukatwa uhusiano huo. Kimsingi Qatar ni kati ya nchi za Kiarabi zinazojaribu kuwa na mahusiano mema na nchi zote za eneo la Asia Magharibi; siasa ambazo imekuwa ikizitekeleza hususan mkabala na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa kadiri kwamba, Doha haikuwa tayari hata kupunguza uhusiano wake na Tehran wakati ilipokuwa chini ya mashinikizo ya nchi nne za Kiarabu yaani Saudia, Misri, Bahrain na Imarati zilizoitaka ikate uhusiano wake na Iran. 

Nukta ya pili ni kuwa, kwa kutekeleza siasa za ustahamilivu wa kimkakati, serikali ya Qatar haikusalimu amri mbele ya mashinikizo kutoka nje, na ilifanya jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba inaibuka mshindi mbele ya mashinikizo hayo. Qatari iliibuka mshindi mbele ya nchi kama Saudia na Misri zinazotambuliwa kuwa miongoni mwa nchi kubwa za Kiarabu. Hata hivyo uhusiano kati ya Qatar, Bahrain na Imarati bado unayumbayumba, sababu kuu ikitajwa kuwa ni kuendelea mivutano kati ya pande hizo.