Wayemeni zaidi ya elfu moja huaga dunia kwa njaa kila wiki
Wananchi wa Yemen zaidi ya elfu moja hupoteza maisha kwa njaa na utapiamlo kila wiki nchini humo.
Taasisi za kimataifa zinazofanya kazi huko Yemen leo zimewasilisha taarifa pambizoni mwa mkutano wa 76 wa kila mwaka wa Baraza Kuu la UN mjini New York na kusisiza kuwa, kila siku mamilioni ya Wayemeni wanapambana ili kubaki hai.
Martin Griffiths Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Anayehusika na Masuala ya Kibinadamu amesema kuwa, uchumi wa Yemen umefikia kiwango kipya cha kuanguka. Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) amebainisha kuhusu hali ya Wayemeni milioni 11 na laki tatu ambao wanahitaji misaada ya kibinadamu ili kusalia hai.
Afisa wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) pia ameeleza kuwa, kupungua mgawo wa chakula mwakani huenda kukapelekea kuaga dunia watoto laki nne wa Yemen walio na umri chini ya miaka mitano iwapo katika muda wa miezi sita ijayo shirika hilo halitapatiwa kiasi cha dola milioni 800.
Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi makubwa ya kivamizi dhidi ya wananchi wa Yemen kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, madola mengine ya kibeberu ya Marekani na kwa ushirikiano mkubwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Kiarabu kama Sudan.
Taasisi za Umoja wa Mataifa likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Unicef zimetahadharisha mara kadhaa kuwa watu wa Yemen wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakuna na nchi hiyo inakaribia kukumbwa na maafa makubwa ya kibinadamu kuwahi kushuhudiwa katika karne iliyopita kufuatia kuendelea mashambulizi mtawalia ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen.