Mashirika ya Umoja wa Mataifa: Utapiamlo kwa watoto umekithiri nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i75480-mashirika_ya_umoja_wa_mataifa_utapiamlo_kwa_watoto_umekithiri_nchini_afghanistan
Imeelezwa kuwa, hali ya kutokuwa na uhakika wa kupata chakula na vita nchini Afghanistan vimeongeza maradufu tatizo la utapiamlo kwa watoto katika nchi hiyo, na hivyo kuzusha wasiwasi mkubwa kwa hatima ya watoto hao pamoja na familia zao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 07, 2021 04:16 UTC
  • Mashirika ya Umoja wa Mataifa: Utapiamlo kwa watoto umekithiri nchini Afghanistan

Imeelezwa kuwa, hali ya kutokuwa na uhakika wa kupata chakula na vita nchini Afghanistan vimeongeza maradufu tatizo la utapiamlo kwa watoto katika nchi hiyo, na hivyo kuzusha wasiwasi mkubwa kwa hatima ya watoto hao pamoja na familia zao.

Hayo yameelezwa na mashhirika ya Umoja wa Mataifa ya Mfuko wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambayo kwa pamoja yametoa wito wa kuweko mshikamano na ushirikiano kwa ajili ya kulinusuru taifa hilo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan Hervé Ludovic De Lys, na mwakilishi wa  WFP Mary-Ellen McGroarty ambao wamefanya ziara ya siku mbili kujionea hali halisi wanasema kuwa, bila upatikanaji wa huduma za maji za kuaminika, chakula, huduma za msingi za afya na huduma za lishe, watoto wa taifa hilo na familia zao wanaweka rehani maisha yao.

Mpango wa Chakula Duniani (WFP)

 

Ripoti zinaonyesha kuwa, watu milioni 14 wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa chakula na watoto wanaokadiriwa kuwa milioni 3.2 wenye umri wa chini ya miaka 5 wanatarajiwa kupata ugonjwa wa unyafuzi (kwashakoo) ifikapo mwishoni wa mwaka huu, huku takribani watoto milioni moja wako katika hatari ya kufa na utapiamlo uliokithiri endapo hawatopata matibabu ya haraka.

Hivi karibuni pia, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu, (OCHA) ilitangaza kuwa, mamilioni ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya chakula pamoja na huduma za kiafya na kwamba, kwa sasa sekta ya utoaji huduma nchini Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya na imo katika hatua ya kusambaratika.