Waziri Mkuu wa Yemen: Mipango michafu ya Israel Asia Magharibi imefeli
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen ametoa pongezi kwa kukombolewa maeneo kadhaa ya Yemen yaliyokuwa chini ya udhibiti wa vikosi mamluki na kueleza kwamba, mipango michafu ya utawala haramu wa Israel pamoja na njama zake Asia Magharibi zimefeli na kugonga ukuta.
Dakta Abdel-Aziz bin Habtour amesema hayo kwa mnasaba wa sherehe za miaka 58 ya "Mapinduzi ya Oktoba 14" na kusisitiza kwamba, mipango ya Kizayuni imefeli ikiwa ni natija ya vipigo mtawalia vya mhimili wa muqawama na kwamba, hivi sasa utawala huo ghasibu umechanganyikiwa na umo katika hali ya kusambaratika.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen ameeleza kuwa, vibaraka na mamluki walioko katika miji mikuu ya baadhi ya mataifa ndio wanaohusika na kusukuma mbele gurudumu la mpango wa Kizayuni wa kuigawa Yemen na eneo la Asia Magharibi kwa ujumla.
Wakati huo huo, msemaji wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amezikosoa vikali asasi na jumuiya za kimataifa kuhusiana na misaada yao ya kibinadamu huko katika Wilaya ya al-Abdiyah katika mji wa Ma'rib na kwamba, hazina nia ya dhati ya kupatia ufumbuzi matatizo ya kibinadamu katika eneo hilo.
Haya yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni wanajeshi wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia wajisalimisha kwa wanamapambano wa Ansarullah katika wilaya ya Al-Abdiyah, kusini mwa mkoa wa Ma'rib.
Mwezi Machi mwaka 2015, Saudi Arabia na waitifaki wake walianzisha mashambulio na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen uliosababisha vifo vya makumi ya maelfu ya raia, kuteketeza miundombinu na kuiwekea mzingiro nchi hiyo masikini ya Kiarabu, lakini kutokana na muqawama wa wananchi wa Yemen, hadi sasa wameshindwa kufikia malengo ya uvamizi wao huo.