UNICEF: Mfumo wa afya na huduma za kijamii Afghanistan zinakaribia kusambaratika
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ametangaza kuwa, mfumo wa afya na huduma za kijamii nchini Afghanistan unakaribia kusambaratika.
Omar Abdi Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) amesema kuwa, sekta ya afya na huduma za kijamii nchini Afghanistan inakabiliwa na ukata mkubwa wa dawa.
Kadhalika afisa huyo wa UNICEF ameeleza kuwa, Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa huduma muhimu na kwamba, watoto wa nchi hiyo ambao hawana hatia yoyote ndio wahanga wakuu wa hali hiyo.
Hayo yanaripotiwa huku kukiweko na taarifa mbalimbali zinazoonyesha kuwa, Afghanistan inakaribia kukumbwa na janga la kibinadamu.
Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF alisema hivi karibuni kwamba, karibu watoto milioni 10 nchini Afghanistan wanahitaji misaada ya kibinadamu ili waweze kubaki hai.
Inaelezwa kuwa, hali ya kutokuwa na uhakika wa kupata chakula na machafuko nchini Afghanistan vimeongeza maradufu tatizo la utapiamlo kwa watoto katika nchi hiyo, na hivyo kuzusha wasiwasi mkubwa kwa hatima ya watoto hao pamoja na familia zao.
Kwa upande wake, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu, (OCHA) inasema kuwa, mamilioni ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya chakula pamoja na huduma za kiafya na kwamba, kwa sasa sekta ya utoaji huduma nchini Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya na imo katika hatua ya kusambaratika kabisa.