WFP yaitolea wito jamii ya kimataifa kumaliza tatizo la njaa Yemen
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) jana umetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuhitimisha tatizo la njaa huko Yemen.
Mpango wa Chakula Duniani wenye mfungamano na Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa umedhamiria kuzisaidia familia za Wayemeni wanaohitaji misaada ya chakula ili kuendelea kuishi. WFP awali ilitangaza kuwa, Yemen inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa chakula duniani. Martin Griffiths Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu pia hivi karibuni aliitaja hali ya kibinadamu huko Yemen kuwa majanga na kueleza kuwa Wayemeni milioni 5 wanakaribia kukumbukwa na hatari ya njaa.
Katika miaka 6 ya karibuni Yemen imeathirika na tatizo la uhaba mkubwa wa mafuta, chakula na suhula za kitiba kutokana na kuzingirwa nchi hiyo kwa pande zote na muungano vamizi unaaongozwa na Saudia.
Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa zilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen Machi 2015 na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, anga, na nchi kavu. Vita hivyo aidha hadi sasa vimeuwa makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.