Mbunge wa Kuwait kuishtaki Saudia kwa kuendeleza ugaidi Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i7594-mbunge_wa_kuwait_kuishtaki_saudia_kwa_kuendeleza_ugaidi_mashariki_ya_kati
Mbunge mmoja wa Kuwait amebuni muungano utakaowaleta pamoja wanasheria wa kimataifa na watetezi wa haki za binadamu kwa lengo la kuishtaki serikali ya Saudi Arabia kwa kuendeleza na kuunga mkono harakati za kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kote kwa ujumla.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2016 11:57 UTC
  • Mbunge wa Kuwait kuishtaki Saudia kwa kuendeleza ugaidi Mashariki ya Kati

Mbunge mmoja wa Kuwait amebuni muungano utakaowaleta pamoja wanasheria wa kimataifa na watetezi wa haki za binadamu kwa lengo la kuishtaki serikali ya Saudi Arabia kwa kuendeleza na kuunga mkono harakati za kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kote kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na tovuti ya shirika la habari la Naba News, Mbunge huyo kwa jina Abdul-Hamid Dashti, amesema lengo la muungano huo ni kutetea maslahi ya wahanga wa mashambulio ya kigaidi ambayo yanaaminika kuwa yana mkono wa utawala wa Aal-Saud.

Mbunge huyo amesema yeye binafsi ndiye atakayeufadhili muungano huo wa wataalamu na wanasheria wa kimataifa kwa shabaha ya kuishtaki serikali ya Riyadh. Amesema lengo lake kuu ni kuionyesha dunia sura na mafunzo halisi ya Uislamu sambamba na kuwatambulisha wahanga wa mashambulizi yaliyofanywa au kufadhiliwa na Saudia.

Hatua ya mbunge huyo inajiri siku chache baada ya Bunge la Seneti la Marekani kupasisha muswada wa sheria itayowapa idhini wahanga wa shambulizi la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani kuchukua hatua za kisheria dhidi ya serikali ya Riyadh.

Hata hivyo muswada huo unasubiri baraka za Bunge la Wawakilishi la nchi hiyo na sahihi ya Rais Barack Obama ili iwe sheria.

Muswada huo umeongeza mashinikizo kwa serikali ya Washington kutakiwa kuweka wazi nyaraka za "kurasa 28" kuhusu tukio la Septemba 11.

Shirika la Ujasusi la Marekani CIA hivi karibuni lilisema ni makosa kuziweka hadharani nyaraka za siri za kurasa 28 kuhusu tukio la Septemba 11, kwa sababu taarifa zake si za uhakika.