Misaada mingine ya Shirika la Afya Duniani (WHO) yawasili Kabul, Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i76678-misaada_mingine_ya_shirika_la_afya_duniani_(who)_yawasili_kabul_afghanistan
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, misaada yake mingine inayojumuisha suhula na zana za kitiba kwa ajili ya kuwahudumia watoto 5,000 imewasili katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul.
(last modified 2026-08-11T03:40:48+00:00 )
Nov 08, 2021 07:50 UTC
  • Misaada mingine ya Shirika la Afya Duniani (WHO) yawasili Kabul, Afghanistan

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, misaada yake mingine inayojumuisha suhula na zana za kitiba kwa ajili ya kuwahudumia watoto 5,000 imewasili katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul.

Shirika la Afya Duniani (WHO) sambamba na kuishukuru serikali ya Qatar kwa ushirikiano iliyotoa limesema kuwa, misaada hiyo itasadia pakubwa kutoa huduma kwa watoto 5,000 Afghanistan ambao wanakabiliwa na maradhi mbalimbali.

Kwa mujibu wa shirika hilo, tangu kuanguka serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghan nchini Afghanistan na wanamgambo wa Taliban kuchukua hatamu za uongozi, Shirika la Ndege la Qatar 'Qatar Airways' limetuma ndege nne nchini Afghanistan kwa ajili ya kupeleka misaada ya tani 60 kwa ajili ya sekta ya afya.

Mwezi uliopita wa Oktoba Omar Abdi Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) alitangaza kuwa, mfumo wa afya na huduma za kijamii nchini Afghanistan unakaribia kusambaratika.

 

Ripoti mbalimbali zimekuwa zikionyesha kuwa, Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa huduma muhimu na kwamba, watoto wa nchi hiyo ambao hawana hatia yoyote ndio wahanga wakuu wa hali hiyo.

Kwa upande wake, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu, (OCHA) inasema kuwa, mamilioni ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya chakula pamoja na huduma za kiafya na kwamba, kwa sasa sekta ya utoaji huduma nchini Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya na imo katika hatua ya kusambaratika kabisa.