Hisham Abu Hawwash ashinda katika mapambano ya kugoma kula chakula
Ushindi wa Hisham Abu Hawwash mateka wa Kipalestina katika vita yake ya kugoma kula chakula mkabala na utawala wa Kizayuni umepokelewa na wimbi la furaha na pongezi kutoka kwa wananchi na makundi ya muqawama ya Palestina na kukiri Wazayuni kuwa wameshindwa kukabiliana na muqawama wa Palestina.
Shirika la habari la Abu Hawwash alikuwa amegoma kula chakula kwa muda wa siku 141 zilizopita akiwa ameshikiliwa katika jela ya utawala wa Kizayuni; na makundi ya muqawama katika siku za karibuni mara kadhaa yaliutahadharisha utawala wa Kizayuni kuhusu athari zitakazoupata iwapo aaga dunia na jibu na kijeshi litakalotolewa na muqawama.
Hatimaye vyombo vya habari vya Palestina jana usiku vilitangaza kuhusu kusalimu amri utawala wa Kizayuni na kukubali kumuachia huru Abu Hawwash Februari 26 ijayo; na kwa utaratibu huo mateka huyo wa Kipalestina ambaye hivi karibuni madaktari wake walidhani kuwa angeaga dunia wakati wowote ule hatimaye amehitimisha mgomo wake huo wa kula.
Baada ya kutangazwa habari hiyo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa taarifa na kutangaza kuwa: harakati hiyo inatoa mkono wa pongezi kufuatia ushindi huo wa Abu Hawwash kwa walinda jela wa Kizayuni katika vita vya watu wenye njaa.
Harakati ya Hamas imesisitiza kuwa mateka huyo shujaa kwa mara nyingine tena amethibitisha nguvu ya Palestina kwa ajili ya muqawama na ushindi dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni na kuwa na azma na irada kubwa ya kutosalimu amri mbele ya Maghasibu.
Wakati huo huo harakati ya Jihad Islami imetoa taarifa na kuwapongeza wananchi wa Palestina kwa mshikamano wao na kumuunga mkono Hisham Abu Hawwash hadi kupatikana ushindi dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni.