UN: Mamillioni ya Wayemen wanakabiliwa na baa la njaa
Umoja wa Mataifa unasema mamilioni ya watu wa Yemen wanakabiliwa na njaa huku misaada ya chakula ikipungua.
Katika taarifa kupitia Twitter, Kamisheni ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa (UNHCR) imesema familia zilizofurushwa makwao Yemen zinakabiliwa na baa la njaa kutokana na kupungua misaada ya chakula.
Taarifa hiyo imesema nusu milioni ya wakimbizi wa ndani nchini Yemen wanaishi katika maeneo ambayo yametajwa kuwa yenye kuhitajia msaada wa dharura wa chakula.
UNCHR inasema mwezi Januari mamilioni ya Wayemen watapokea msaada uliopungua wa chakula kutokana na kupungua misaada ya kimataifa ya misaada.
Vita vilivyoanzishwa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen kuanzia Machi 2015 na kuendelea hadi sasa vimeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha wengine milioni nne wakiwa hawana pa kuishi. Aidha vita hivyo vimesababisha matatizo mengi ya ukosefu wa chakula, matibabu na elimu kwa watu wa Yemen.
Uchokozi na uvamzi wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen umebomoa na kuharibu zaidi ya asilimia 85 ya miundombinu ya nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu na kuisababishia pia uhaba mkubwa wa chakula na dawa.
Hivi karibuni Muhammad Ali al-Huthi, mwanachama wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amekosoa utendaji wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya kivamizi dhidi ya nchi hiyo na kusema licha ya kwamba Saudi Arabia imetekeleza na inaendelea kutekeleza jinai za kivita nchini humo, lakini baraza hilo limeshindwa kusimamisha vita hivyo.