San'a: Njama za Marekani nchini Yemen hazina mustakbali wowote
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i79442-san'a_njama_za_marekani_nchini_yemen_hazina_mustakbali_wowote
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, njama za Marekani hazina mustakbali wowote nchini humo na huo ndio ujumbe uliomo kwenye operesheni za jeshi la Yemen na kamati za kujitolea na za ukombozi za wananchi wa nchi hiyo.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jan 21, 2022 04:30 UTC
  • San'a: Njama za Marekani nchini Yemen hazina mustakbali wowote

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, njama za Marekani hazina mustakbali wowote nchini humo na huo ndio ujumbe uliomo kwenye operesheni za jeshi la Yemen na kamati za kujitolea na za ukombozi za wananchi wa nchi hiyo.

Televisheni ya al Masirah imemnukuu Ali al Qahum akisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo vinatumia uwezo wao wote kwa ajili ya mapambano na kuzuia mashambulizi na kwamba katika upande wa kisiasa pia operesheni za vikosi vya ulinzi vya Yemen zinapokewa vizuri.

Ameongeza kuwa, adui leo hii amelazimika kutia mkono kizani kwa kushirikiana na magenge ya kigaidi ya Daesh (ISIS) na al Qiada kwa tamaa kuwa magenge hayo ya ukufurishaji yanaweza kuwaokoa wavamizi hao wa Yemen na hiyo ni karata ya mwisho ya adui ndani ya ardhi ya Yemen ambayo nayo karibuni hivi itasambaratishwa kikamilifu.

Mapambano ya wananchi wa Yemen ya ukombozi wa ardhi zao

 

Kiongozi huyo mwanadamizi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen pia amesema, vikosi vya Yemen vimeonesha hamasa kubwa katika medani za mapambano na vimetoa ujumbe maalumu kwa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Saudi Arabia na Marekani kwamba kutegemea kwao magenge ya wakufurishaji ni kosa jingine kubwa katika faili jeusi la jinai zao.

Amesema, tangu wavamizi walipoivamia Yemen na kuanza kufanya ukatili dhidi ya wananchi wa nchi hiyo hadi hivi sasa, muda wote wamekuwa wakifanya jinai zisizo na kifani dhidi ya raia, lakini hivi sasa viongozi wa Yemen wameweza kuwa na mikakati maalumu ya kupambana na adui na kulinda wananchi wao.