Nasrullah: Hizbullah ina uwezo wa kuunda ndege zisizo na rubani
-
Sayyid Hassan Nasrullah
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah amesema harakati hiyo sasa inajiundia ndege zisizo na rubani au drone na makombora yenye uwezo wa kulenga shabaha kwa umakini mkubwa.
Akizungumza kwa njia ya televisheni Jumatano ya jana, Sayyid Nasrullah alisema Hizbullah imeweza kupata mafanikio hayo kwa kujitegemea na kuongeza kuwa, “tumekuwa tukiunda drone kwa muda mrefu nchini Lebanon na yeyote anayetaka tunaweza kumuuzia.”
Amesema Hizbullah ina utaalamu wa kuimarisha uwezo wa maroketi yake kukabiliana na tishio la Israel. Kiongozi wa Hizbullah ameyasema hayo kwa mnasaba wa kukumbuka kuuawa shahidi viongozi wa harakati ya mapambano ya Kiislamu Sheikh Ragheb Harb, Sayyid Abbas al-Mousawi and Imad Mughniyeh.
Sayyid Nasrullah amesema, tangu mwaka 1982 harakati ya Hizbullah imekuwa ikilinda Lebanon kwa kukabiliana na vitisho vya Israel.
Aidha amezilaani nchi za Waislamu ambazo zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kuutaja utawala huo kuwa ni ‘utawala wa muda’ ambao unaelekea kusambaratika.
Vilevile amesema Israel ni utawala pekee duniani ambao sasa unajulikana kama utawala wa apartheid huku akisema maafisa wa utawala huo wamekiri kuwa wanakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha utawala huo unaendelea kuwepo.