Jihadul Islami: Israel ni 'mwanaharamu' wa ukoloni wa Magharibi
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imeutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kama mwanaharamu wa ubeberu na ukoloni wa nchi za Magharibi.
Haitham Abu al-Ghazlan, Katibu Mkuu wa harakati hiyo ya muqawama katika mahojiano na shirika la habari la Al-Ahd ameashiria safari ya Isaac Herzog, rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Uturuki na kueleza kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na adui ni kuwasaliti wananchi wa Palestina.
Al-Ghazlan amelaani vikali ziara hiyo ya rais wa utawala pandikizi wa Israel nchini Uturuki na kusisitiza kuwa, Israel ni mtoto wa nje ya ndoa wa sera za ukoloni.
Aidha Youssef al-Husseini, mwanachama wa tawi la kisiasa la Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina ameutaja utawala huo haramu kuwa mwanaharamu wa ukoloni wa Wamagharibi.
Naye Kayed al-Ghul, mwanachama wa tawi la kisiasa la Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina (PFLP) amesema, licha ya taharuki za kisiasa baina ya Uturuki na utawala wa Kizayuni katika nyakati tofauti huko nyuma, lakini ushirikiano wa pande mbili hizo katika nyuga za uchumi, diplomasia na usalama haukukatika.
Amesema sera za Uturuki zinakinzana, na ni kwa sababu hiyo katika vyombo vya habari Ankara inajionyesha kuwa muungaji mkono mkubwa wa Palestina, lakini kivitendo inafanya kinyume chake.