Bin Salman atumia mafuta kuishinikiza Magharibi iiruhusu Saudia iendelee kunyonga watu
Tovuti ya habari ya Middle East Eye imeripoti kuwa, Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia anazinishiniza nchi za Magharibi zikubali Saudia iendelee kunyonga watu na kufanya inavyotaka mkabala wa mafuta ya petroli.
Katika makala iliyochapishwa na Middle East Eye, Mwanamfalme wa Saudi Arabia na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Muhammad Bin Salman anavuna faida kutokana na utegemezi wa nchi za Magharibi kwa mafuta ya bei rahisi ya Saudia; wakati huu ambapo bei ya mafuta ya petroli inazidi kuongezeka duniani kutokana na operesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine.
Makala hiyo imeeleza kuwa, utawala wa ukoo wa Aal Saud umetumia vibaya fursa ya kushughulishwa dunia na vita vya Ukraine na kupanda kwa bei ya petroli duniani, kutekeleza hukumu za kunyonga watu kwa umati.
Jumamosi ya wiki iliyopita, utawala wa Kifalme wa Saudia uliwanyonga watu 81 wakiwemo vijana 41 Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mauaji hayo ya wafungwa wa itikadi na mateka wa vita yametajwa kuwa ndiyo makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kufanyika ndani ya siku moja katika historia ya Saudi Arabia.
Watu wengine watatu walinyongwa na Riyadh Jumatano iliyopita, siku ambayo Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson aliitembelea Saudia kwa shabaha ya kuushawishi utawala huo wa kifalme uongeze kiwango cha uzalishaji wa mafuta ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo inayozidi kuongezeka duniani kutokana na mgogoro wa Ukraine.
Makala hiyo iliyochapishwa na Middle East Eye imeeleza kuwa, Bin Salman anatumia fursa hii (mgogoro wa Ukraine) kutunisha misuli yake, na kuwashinikiza Wamagharibi wamheshimu, baada ya kumtazama kwa jicho la dharau kwa miaka mitatu.