Matukio ya Kisiasa na Kimedani Iraq
Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al Abadi ambaye pia ni amiri jeshi mkuu nchini humo jana alitangaza kukamilika duru za kwanza na ya pili za kuukomboa mji wa Fallujah ambao unakaliwa kwa mabavu na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).
Imearifiwa kuwa, siku ya Jumatano aliingia katika kituo cha oparesheni za kuukomboa mji wa Fallujah na akafahamishwa kuhusu hatua zilizochukuliwa za kukabiliana na kundi la ISIS. Kabla ya hapo Salim al Jabouri Spika wa Bunge la Iraq pia alitembelea kituo hicho cha kijeshi. Duru zinadokeza kuwa jeshi la Iraq limepunguza kasi ya oparesheni ya kuukomboa mji wa Fallujah ili kuzuia mauaji ya raia ambao wanatumiwa kama ngao ya kibinadamu na magaidi wa ISIS.
Huku hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Iraq amesema vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa kusambaratisha makundi kadhaa ya kigaidi mjini Baghdad ambayo yalikuwa yanapanga njama za kutekekeza njama za kuwadhuru raia.
Haidar al Abadi pia amewasilisha mpango utakaotekelezwa baada ya mji wa Fallujah kukombolewa ikiwa ni pamoja na kurejesha usalama, kuwarejesha wakimbizi waliokimbia na kuujenga upya mji huo. Aidha amevipongeza vikosi vya Iraq kwa kukomboa maeneo yote ya karibu na Fallujah.
Vikosi vya Iraq vinatekeleza oparesheni kubwa ya kuwatimua magaidi wa ISIS kutoka mji wa Fallujah ulio kilomita 60 kutoka Baghdad. Mji huo ni kituo kikubwa zaidi cha ISIS nchini Iraq.
Baada ya kupita siku kadhaa za oparesheni za kuukomboa mji huo ulio katika mkoa wa Al Anbar, vikosi vya Iraq sasa vinakabiliana na magaidi wa ISIS katika vita vya ana kwa ana mitaani mjini humo.
Vikosi vya Iraq pia vimekata mawasiliano ya barabara baina ya mji wa Fallujah na mji wa Saqlawiyah ambao ulikuwa na nafasi muhimu ya kuwafikishia magaidi wa ISIS misaada ya kivita.
Hivi sasa baada ya kupata pigo magaidi wa ISIS mbele ya jeshi la Iraq na vikosi vya wananchi, magaidi hao sasa wamekithirisha hujuma zao katika mji mkuu, Baghdad na maeneo mengine ya Iraq.
Hii ni katika hali ambayo katika kikao cha dharura cha Bunge la Iraq, suala la usalama na uchumi lilijadiliwa kwa kina siku ya Jumanne chini ya usimamizi wa spika Salim al Jabouri.
Bunge la Iraq lilikuwa limefungwa kwa muda wa mwezi mmoja kutokana na matukio ya Aprili 20 na Mei 20 ambapo wapinzani walihujumu jengo la bunge wakitaka waziri mkuu ajiuzulu.
Viongozi wa Iraq wametoa wito wa kuwepo umoja wa kitaifa katika kipindi hiki ambapo nchi hiyo inatekeleza oparesheni za kuwaangamiza magaidi wa ISIS.