Amir wa Qatar amshukuru Rais wa Iran kwa mapokezi mazuri
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i83558-amir_wa_qatar_amshukuru_rais_wa_iran_kwa_mapokezi_mazuri
Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter ambapo amemshukuru Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mapokezi mazuri na ukarimu wakati wa ziara yake mjini Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2022 03:15 UTC
  • Amir wa Qatar amshukuru Rais wa Iran kwa mapokezi mazuri

Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter ambapo amemshukuru Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mapokezi mazuri na ukarimu wakati wa ziara yake mjini Tehran.

Kiongozi huyo wa Qatar aliwasili Tehran Alhamisi asubuhi akiongoza ujumbe wa ngazi za juu kisiasa na kiuchumi ambapo amekutana na viongoziw a ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika ujumbe wake wa Twitter, Amir wa Qatar ametuma picha akiwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuandika: "Namshukuru Mheshimiwa Rais Ibrahim Raisi kwa mapokezi mazuri na ukarimu wakati wa ziara yangu Tehran, ambayo ilijumuisha majadiliano na Mheshimiwa Rais kuhusu masuala ya kuunga mkono ushirikiano wa nchi zetu mbili katika nyanja mbalimbali. Pia tulijadili njia za kuimarisha usalama na uthabiti wa eneo kwa kuzingatia maendeleo ya sasa ya kikanda na kimataifa."

Akizungumza jana katika kikao cha pamoja na waandishi habari akiwa ameandamana na Rais wa Iran, Amir wa Qatar alisema uhusiano wa nchi hizi mbili ni imara na umejeingeka katika misingi ya ujirani mwema.

Ujumbe wa Twitter wa Amir wa Qatar

Aidha kiongozi huyo wa Qatar amebainisha kwamba, katika mazungumzo yake na Rais Ebrahim Raisi, wametilia mkazo juu ya kupatiwa ufumbuzi matatizo mbalimbali yanayolikabili eneo la Asia Magharibi kupitia njia ya mazungumzo.

Amir wa Qatar pia alikutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei. Katika kikao hicho, Amir wa Qatar alibainisha furaha aliyokuwa nayo kwa kuitembelea Iran. Huku akiashiria uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Qatar amesema: "Kamati ya uchumi baina ya nchi mbili sasa inafanya kazi na mwaka ujao ushirikiano wa kiuchumi utaongezeka kwa kiwango kikubwa."