Sheikh Naim Qassem: Hizbullah iko tayari kuwazuia Wazayuni wasianzishe uchimbaji gesi
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, ikiwa serikali itatoa agizo, harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu iko tayari kuchukua hatua yoyote dhidi ya operesheni za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel za kuchimba gesi katika maeneo yanayozozaniwa kati ya utawala huo na Lebanon.
Siku ya Jumapili, utawala wa Kizayuni ulivuka mpaka wa baharini wa Lebanon na kuweka jukwaa la gesi katika Bahari ya Mediterania na umepanga kufunga jukwaa la kuvutia gesi katika eneo la Karish ili kulitumia kwa ajili ya ugunduzi na uchimbaji gesi katika eneo hilo.
Televisheni ya Al Manar imeripoti kuwa, Sheikh Naim Qassem, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, ikiwa serikali ya Lebanon itatangaza rasmi kwamba utawala wa Kizayuni umekiuka mipaka ya baharini ya nchi hiyo, harakati hiyo ya muqawama iko tayari kuchukua hatua yoyote dhidi ya operesheni za utawala haramu wa Israel za kuchimba gesi katika maeneo yanayozozaniwa na utawala huo na Lebanon.
Sheikh Naim Qassem ametamka bayana kwamba, pale serikali ya Lebanon itakapotangaza kuwa utawala wa Kizayuni unapora maji na mafuta ya nchi, Hizbullah itakuwa tayari kutumia nyenzo mwafaka kuzuia wizi wa wazayuni wa kupora utajiri wa mafuta na gesi ya Lebanon.
Kabla ya hapo Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri naye pia alizungumzia hujuma ya utawala haramu wa kizayuni wa Israel dhidi ya mamlaka ya baharini ya nchi hiyo ya Kiarabu katika Bahari ya Mediterania na akasisitiza kwamba, Lebanon haitakubali katu kunyamazia kimya hatua na hujuma hizo.
Rais Michel Aoun na Najib Miqati, waziri mkuu wa muda wa Lebanon nao pia katika nyakati tofauti walishatoa onyo kwa utawala haramu wa Kizayuni juu ya chokochoko zozote unazofanya katika eneo la majini linalozozaniwa na pande hizo mbili, wakisisitiza kuwa Lebanon inazichukulia chokochoko hizo kuwa ni hatua ya uhasama na uadui.../