Waziri Mkuu wa Israel afanya safari ya kushtukiza Imarati
Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel yupo Abu Dhabi katika ziara rasmi ya kuutembelea Muungano wa Falme za Kiarabu.
Hii ni mara ya pili kwa Bennett kuitembelea Abu Dhabi, tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanzishe uhusiano wa kawaida na Imarati mwishoni mwa mwaka 2020.
Ofisi ya Bennett imesema Waziri Mkuu huyo wa Israel anakutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa UAE, akiwemo rais wa Imarati, Mohammed bin Zayed Aal Nahyan.
Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imesema wawili hao wanatazamiwa kuzungumzia masuala mbalimbali ya kieneo, huku kadhia ya Iran ikiwa ajenda kuu ya mazumgumzo yao.
Mapema mwaka huu, Isaac Herzog, rais wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, alienda mjini Abu Dhabi katika safari ya kwanza rasmi ya kuutembelea Muungano wa Falme za Kiarabu.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, hatua ya Imarati ya kuwapokea kwa mikono miwili wakuu wa utawala pandikizi wa Israel ni kuendeleza hatua zake dhidi ya taifa la Palestina na katika kivuli cha kudumishwa vitendo vya mabavu vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Disemba mwaka 2020, Imarati ilisaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Mapatano hayo yalisainiwa katika Ikulu ya White House na kuhudhuriwa na rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump.