HAMAS na Jihadul-Islami: Muqawama ndio njia pekee ya kuikomboa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i84664-hamas_na_jihadul_islami_muqawama_ndio_njia_pekee_ya_kuikomboa_palestina
Harakati za Hamas na Jihadul Islami za Palestina zimelaani vikali mwenendo wa baadhi ya watawala wa Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kusisitiza kwamba, muqawama ndio njia pekee ya kuzikomboa ardhi za Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2022 06:07 UTC
  • HAMAS na Jihadul-Islami: Muqawama ndio njia pekee ya kuikomboa Palestina

Harakati za Hamas na Jihadul Islami za Palestina zimelaani vikali mwenendo wa baadhi ya watawala wa Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kusisitiza kwamba, muqawama ndio njia pekee ya kuzikomboa ardhi za Palestina.

Sisitizo hilo limetolewa katika mazungumzo baina ya maafisa kadhaa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Jihadul Islami walipokutana mjini Beirut mji mkuu wa Lebanon katika hauli na kumbukumbu ya mwaka wa pili tangu alipoaga dunia Ramadhan Abdallah Shalah, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jihadul Islami.

Viongozi hao wa Hamas na Jihadul-Islami wamelaani vikali uvamizi wa mara kwa mara wa Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina katika mji mtakatifu wa Quds, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na dhidi ya ardhi za Palestina zilizoghusubiwa na kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948.

 

Ihsan Ataya, mwakilishi wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina nchini Lebanon na Ali Baraka, mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon wameyataka makundi yote ya Palestina kudumisha umoja na mshikamano baina yao ili kuimarisha safu ya kupambana na Wazayuni wavamizi.

Aidha viongozi hao sambamba na kulaani mwenendo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel wameyataka mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kukata uhusiano wao wa aina yoyote ile na utawala ghasibu wa Israel, na kufanya juhudi kadiri inavyowezekana kuuwekea utawala huo bandia vikwazo vya kimataifa ili kuulazimisha usitishe jinai, ugaidi na uvamizi wake dhidi ya taifa la Palestina na matukufu ya Kiislamu.