Viongozi wanane wa magaidi wa ISIS waangamizwa kaskazini mwa Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i84758-viongozi_wanane_wa_magaidi_wa_isis_waangamizwa_kaskazini_mwa_iraq
Vikosi vya kulinda usalama vya Iraq vimeshambulia maficho ya magaidi wa Daesh (ISIS) katika mkoa wa Salahuddin wa kaskaizni mwa nchi hiyo na kuangamiza viongozi wasiopungua wanane wa genge hilo la ukufurishaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2022 02:59 UTC
  • Viongozi wanane wa magaidi wa ISIS waangamizwa kaskazini mwa Iraq

Vikosi vya kulinda usalama vya Iraq vimeshambulia maficho ya magaidi wa Daesh (ISIS) katika mkoa wa Salahuddin wa kaskaizni mwa nchi hiyo na kuangamiza viongozi wasiopungua wanane wa genge hilo la ukufurishaji.

Licha ya genge hilo kusambaratishwa huko Iraq na Syria, lakini baadhi ya wanachama wa Daesh wamejificha ndani ya jamii na huwa wanafanya mashambulio ya hapa na pale kama majambazi.

Kampeni kubwa inayoendeshwa na vikosi vya ulinzi vya Iraq hivi sasa ni kuhakikisha kuwa genge hilo la ISIS halipati nguvu tena nchini humo na muda wote vikosi hivyo vinafanya operesheni za kuisafisha kabisa Iraq na uwepo wa magaidi hao.

Televisheni ya al Dijla ya Iraq imenukuu taarifa ya kitengo cha habari cha vikosi vya ulinzi vya Iraq ikisema kuwa, muda wote majeshi ya Iraq yanafanya upelelezi wa kina na hivi karibuni wamepata taarifa za uhakika zilizopelekea kuangamizwa viongozi wanane wakubwa wa genge la Daesh wakiwa wamejificha kwenye bonde moja mkoani Salahuddin. 

Genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) lilisambaratishwa nchini Iraq mwezi Nomvemba 2017

 

Taarifa hiyo imesema kuwa, baada ya kupata taarifa hizo za kiintelijensia, ndege za kivita za Iraq zimeshambulia mara tatu maficho hayo na kuwaangamiza viongozi wote wanane wa ISIS waliokuwa wamejificha hapo. Mwaka 2014 na kutokana na msaada mkubwa wa kifedha na kijeshi wa Marekani pamoja na waitifaki wake wa Magharibi na wa Kiarabu kama vile Saudi Arabia, genge la kigaidi la ISIS lilivamia nchi ya Kiarabu ya Iraq na kuteka maeneo mengi ya kaskaizni na magharibi mwa nchi hiyo.

Magaidi hao walifanya jinai kubwa dhidi ya wananchi wa Iraq, jinai ambazo ni mara chache kushuhudiwa katika historia. Serikali ya Iraq iliomba msaada wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baada ya miaka michache, vikosi vya Iraq vilifanikiwa kulisambaratisha genge hilo.

Tarehe 17 Novemba 2017, vikosi vya Iraq vilifanikiwa kuteka mji wa Rawa wa mkoa wa al Anbar. Huo ndio mji wa mwisho uliokuwa unadhibitiwa na magaidi wa Daesh (ISIS) huko Iraq.