Aug 30, 2022 13:00 UTC
  • Muqtada Sadr na machafuko ya Iraq

Jumatatu ya jana tarehe 29 Agosti Iraq ilishuhudia sokomoko na matukio ambayo kimsingi yalitabiriwa kutokea.

Wimbi la machafuko hayo lilienea huku chanzo na chimbuko lake likiwa ni mwenendo wa kisiasa wa Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr ya Iraq. Jumatatu ya jana Ayatullah Hairi Marjaa Taqlidi wa Kishia ambaye anatambuliwa na wengi kama muungaji mkono wa Muqtada Sadr na harakati yake, alitangaza kujivua jukumu la Umarjaa kutokana na sababu za maradhi na uzee. Katika taarifa yake, Ayatullah Hairi alimhutubu Muqtada Sadr kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kukosoa fitina na ufarakishanaji wananchi wa Iraq kwa kutumia majina ya mashahidi wawili wa kizazi cha Sadr, katika hali ambayo hajafikia daraja ya Iijtihad na kutimiza masharti mengine ya lazima na kisha akataka kuchukua hatamu za uongozi wa kisheria, basi mtu huyo atakuwa si katika safu ya kizazi cha Sadr.

Taarifa hiyo ya Ayatullah Hairi ilikabiliwa na radiamali ya haraka ya Muqtada Sadr, ambapo kiongozi huyo wa Harakati ya Sadr sambamba na kumkosoa vikali Ayatullah Hairi, alitangaza kuachana na siasa. Hii si mara ya kwanza kwa Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr kutangaza kujiuzulu shughuli za kisiasa kwani huko nyuma aliwahi kutangaza mara kadhaa uamuzi kama huo, lakini baadaye akarejea katika ulingo wa siasa.

Kuna nukta kadhaa muhimu kuhusiana na machafuko mapya yaliyoibuka Iraq na kupelekea kwa akali watu 20 kuuawa na wengine 350 kujeruhiwa.

Ayatullah Kadhim Hairi

 

Nukta ya kwanza ni kuwa, ilikuwa ikitarajiwa kwamba, Muqtada Sadr ataitumbukiza Iraq katika vurugu na machafuko. Hatua yake ya kutangaza Juni mwaka huu kujiondoa katika harakati za kisiasa, haikuwa na lengo la kutoa mwanya kwa makundi na mirengo ya kisiasa ya Iraq iondoke katika mkwamo wa kisiasa, bali lengo lilikuwa ni kushinikiza wapinzani wake na kuzuia kupatikana nidhamu na mfumo mpya wa kisiasa nchini Iraq akistafidi na maandamano ya barabarani.

Hujuma na mashambulio dhidi ya Bunge na Baraza Kuu la Mahakama katika majuma ya hivi karibuni ni mambo ambayo yanaweza kutathminiwa pia katika uga huu kwamba, Muqtada Sadr anaona kuwa, anaweza kufikia malengo yake kupitia vurugu na machafuko. Katika taarifa yake ya jana Muqtada Sard alitangaza kuachana kabisa na siasa, hata hivyo hakuwataka wafuasi wake wasifanye maandamano na fujo. Kwa maneno mengine ni kuwa, kwa njia isiyo ya moja kwa moja Sadr alikuwa akitaka machafuko na vurugu ziibuke nchini Iraq.

Wafuasi wa Muqtada Sadr

 

Pili ni kuwa, kwa uchache katika kipindi cha wiki moja iliyopita, Muqtada Sadr alifanya mambo nchini Iraq kiasi kwamba, kivitendo akawa amewapoteza waitifaki wake wa kisiasa. Hatua ya Ayatullah Hairi ya kumkosoa Muqtada Sadr ni jambo lililomuongezea mashinikizo kiongozi huyo wa Harakati ya Sadr na kivitendo akajipata yupo katika nafasi ya kudhoofika na kwa namna fulani kujiona amepata pigo, jambo ambalo kwa Muqtada Sadr ni kitu kisichokubalika.

Nukta ya mwisho ni hii kwamba, hatua ya jana na kuibadilisha Iraq kuwa uwanja wa machafuko ya ndani ni jambo lisilokubaliwa kabisa na makundi, mirengo ya kisiasa na shakhsia rasmi wa nchi hiyo wakiwemo waitifaki wa zamani wa Sadr, bali ni makundi yenye chuki tu kama Chama cha Baath na makundi potofu na vilevile mabaki ya kundi la kigaidi la Daesh ndio yanayonufaika na hali hii. Kung'ang'ania kujitokeza barabarani na katika mitaa mbalimbali ya miji ya Iraq, mbali na kusababisha wananchi wa nchi hiyo kuwa wahanga wakuu wa ukaidi wa kisiasa wa Harakati ya Sadr, siyo tu kwamba hakujaweza kudhamini maslahi ya kundi hilo, bali kumeufanya umoja wa ardhi yote ya Iraq ukabiliwe na tishio kubwa.

Tags